Nafuu kubwa wagonjwa wa figo

Nafuu kubwa wagonjwa wa figo

Muktasari:

  •  Mwanga zaidi umeonekana katika matibabu ya figo nchini baada ya Serikali kununua mashine za kusafisha kiungo hicho (dialysis) moja kwa moja kutoka viwandani, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za huduma hiyo kwa asilimia 50.

  

Dar es Salaam. Mwanga zaidi umeonekana katika matibabu ya figo nchini baada ya Serikali kununua mashine za kusafisha kiungo hicho (dialysis) moja kwa moja kutoka viwandani, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za huduma hiyo kwa asilimia 50.

Hatua hiyo inayochukuliwa na Bohari ya Dawa (MSD) inalenga kushusha gharama za huduma hiyo kutoka Sh300,000 na sasa hadi takriban Sh100,000 kila mgonjwa anapopata huduma hiyo ifikapo Januari 2022.

Uwepo wa mashine hizo ambazo tayari zimeshaanza kufungwa katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya, ikiwemo Mafia na Rubya mkoani Kagera, zitaleta ahueni ya punguzo kwa asilimia 47.

Mgonjwa wa figo anayehitaji huduma ya kusafishwa hutakiwa kufanya hivyo kwa vipindi tofauti, wapo wa kila siku, mara tatu kwa wiki na mara tatu kwa wiki.

Machi mwaka huu, Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima alinukuliwa akisema hapa nchini kuna wagonjwa sugu kati ya 4,800 hadi 5,200 wanaohitaji huduma ya kusafisha damu au kupandikizwa figo.

“Kati ya hao, wagonjwa 1,000 wanapata huduma ya usafishaji wa damu kwa sasa.

Watakaofikiwa

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Meja Jenerali Gabriel Mhidize amesema baadhi ya mashine hizo zimeshafika nchini na miongoni mwa hospitali zitakapofungwa ni Muhimbili, Dodoma-UDOM, Sekou-Toure, Mwanza, Chato, Temeke, Amana, Tumbi na Mwananyamala.

“Gharama za dialysis nchini ni kubwa mno, kwa mfano kwa sasa zinakwenda hadi kati ya Sh230,000 na Sh300,000. Mtu wa kawaida hawezi kuzimudu, ina maana mtu akipata tatizo la figo anaandikiwa hati ya kifo mapema, hiyo haikubaliki. Nchi nyingine ni bei nafuu, kwa nini kwetu iwe ghali,” alihoji.

Alisema kufuatia ughali wa huduma, MSD ilitafuta mashine zenye ubora kwa bei nafuu na hivyo waliingia mkataba na watengenezaji wa mashine hizo ambao walikubaliana wanunue idadi kubwa kwa bei nafuu.

“Kwa sasa tumelenga iwe chini ya laki moja na inaweza ikashuka zaidi, kituo cha afya kule Tandahimba kinaweza kitatoa huduma ya dialysis kwa laki moja au chini ya hapo.

“Tumepata mashine na vifaa vya kuchuja damu vyenye ubora wa kimataifa na vimethibitishwa na TMDA, pia zimepungua bei. Zimeshawasili nchini na zimeanza kufungwa na tutaendelea kuongea kwa kushirikiana na wenzetu wa NHIF ili zifungwe hospitali za rufaa za mikoa, huduma hii itapatikana maeneo mengi zaidi kuliko awali,” alisema Meja Jenerali Mhidze bila kutaja gharama za mashine hizo wala idadi yake. Alisema manunuzi hayo ya mashine yataokoa Sh18 bilioni kwa mwaka.

Bei za vipimo chini

Mbali na mashine hizo, Meja Jenerali Mhidze alisema MSD pia imeanza kununua mashine na vifaa vya maabara kwa punguzo la asilimia 50 mpaka 100 na kwamba wanaendelea kuwasiliana na watengenezaji ili gharama hizo zishuke zaidi.

“Ndiyo mwelekeo wa sasa wa NHIF na MSD, tunataka huduma hizi zipatikane kwa bei nafuu. NHIF itavikopesha hivi vituo kwa bei nafuu zaidi, kwa mfano mashine iliyokuwa inauzwa Sh57 milioni itapatikana Sh25 milioni, ya Sh27 milioni itakuwa Sh14 milioni, ya Sh14 milioni itakuwa Sh7 milioni na ya Sh7 milioni itakwenda kwa Sh2 milioni.

“Hii itasaidia badala ya kupima kwa Sh10,000 utapima kwa Sh2,000, kitu ambacho kitakuwa kizuri na kila mtu akapata huduma stahiki katika eneo lake analoishi.”

Waziri Gwajima amesema hadi kufikia Januari mwakani, vituo vya afya vyote nchini vitakuwa na mashine za kisasa za upimaji katika maabara na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

“Matarajio hadi ifikapo Desemba mwaka huu usambazaji wa mashine hizo katika vituo vyote nchini utakuwa umekamilika na ifikapo Januari kila kituo kitaanza kuzitumia, Serikali itatoa tamko rasmi mara usambazaji wake utakapokuwa umekamilika.

“Kupatikana kwa mashine za kutosha katika vituo vyote pia kutawezesha gharama za huduma kushuka, lakini pia kutaondoa ulazima wa wananchi kusafiri umbali mrefu kupata huduma ya vifaa ambavyo pengine hapo awali vilikosekana katika maeneo yao,” aliongeza Dk Gwajima.

Aidha Meja Jenerali Mhidze alisema MSD wamejipanga kikamilifu kuhakikisha mashine hizo zinasambazwa katika vituo vyote nchini kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.

Maandalizi yaanza

Katika hospitali ya Sekou Toure ambako huduma ya kusafisha figo itafanyika, maandalizi yameanza na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Bahati Msaki amesema wiki ijayo huduma itaanza kutolewa.

“Kwa sasa tupo katika ukarabati wa jengo la dialysis na tunatarajia kukamilisha wiki ijayo. Tukimaliza mashine zitaanza kufungwa na tutaanza kutoa huduma hiyo,” alisema.

Akizungumzia huduma hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Yudas Ndungile alisema uwepo wa mashine za kusafisha figo katika ngazi za chini itasogeza huduma karibu na wananchi.

“Kwa Mkoa wa Shinyanga hatuna kituo cha dialysis, inabidi kwenda mpaka Bugando, Mwanza. Hii itawapunguzia wananchi gharama kubwa ya kwenda Mwanza na gharama ya kuishi huko.

“Ikisogezwa mpaka hospitali ya rufaa ya mkoa na halmashauri itawaondolea adha kusafiri umbali mrefu, gharama kubwa nje ya matibabu pamoja na kuishi mbali na makazi,” alisema Dk Ndungile.

Dialysis inavyofanya kazi

Dialysis ya figo ni matibabu ambayo kawaida hujumuisha kutumia mashine, kuchukua kazi ya figo kuchuja sumu, taka na maji kutoka mwilini. Tiba hii huhitajika na wagonjwa ambao figo zao hazifanyi kazi vizuri. Figo hufanya kazi ya kuchuja damu ili kuondoa maji ya ziada na bidhaa taka kwa kuzigeuza mkojo.

“Mgonjwa kabla ya kufika kwenye mashine hutokea wodini, huko madaktari wanathibitisha kwamba huyu anahitaji matibabu ya kuchuja damu, anapoanza tunamfanyia kwa kiwango maalumu atafanya mara tatu mpaka nne kwa siku, baadaye ataanza kufanyiwa kwa shift atapangiwa aje mara tatu kwa wiki,” alisema Mtaalamu wa kitengo cha uchujaji damu kupitia figo bandia ‘dialysis’ Muhimbili, Judith Mwaipopo.

Alisema ndani ya mashine mgonjwa anatakiwa kukaa kwa saa nne, kwani mgonjwa akishafikia hatua ya figo kutokufanya kazi ambazo ilikuwa kutoa sumu, maji machafu, kupunguza maji mwilini, figo haiwezi kufanya kazi zake inabidi itegemee mashine ambayo hufanya kazi za figo. “Figo ikishindwa kupewa huduma hizo, mgonjwa atapoteza maisha kwakuwa atashindwa kupumua, ataongezeka uzito, maji yaliyotakiwa yatoke yote yatabaki mwilini,” alisema.