Naibu Meya ataka makahaba wadhibitiwe Manispaa ya Tabora

Muktasari:

  • Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora, Amran Kasongo amesema wanawake hao wanahatarisha maisha yao na kusababisha wengine kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi ambao jitihada zinafanyika kuuatokomeza.

Tabora. Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora, Amran Kasongo ametaka wanawake wanaojiuza mitaani nyakati za usiku katika Manispaa ya Tabora wadhibitiwe.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani leo naibu meya huyo amesema hali hiyo inahatarisha maisha yao na kusababisha wengine kupata maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi ambao jitihada zinafanyika kuuatokomeza.

Kasongo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Ukimwi, amesema kamati yake imefanya juhudi za kuwaunganisha wanawake katika vikundi na kuwaomba madiwani kuviunga mkono vikundi hivyo ili vipate mikopo ya kuwasaidia kupata kipato mbadala.

"Tumejitahidi kuunganishwa katika vikundi hivyo tunaomba mtuunge mkono wapate mikopo ili waachane na Yale yasiyofaa," amesema.

Ameielezea kamati yake kuwa unafanya Kila jitihada kuhakikisha maambukizi mapya hanapungua katika Manispaa ya Tabora na kupongeza Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa namna wanavyoshirikiana vizuri kuwasaidia makahaba.

Awali muuguzi wa Town Kliniki, Grace Sinda aliwaeleza madiwani kuwepo ongezeko la wasichana wanaojiuza katika manispaa hiyo.

Amesema wanapata wakati mgumu kwa vile wanajitahidi kutoa elimu kuhusu athari za Ukimwi wakati wasichana na wavulana wanaojiuza kwenye Mitaa.

"Kama tusipodhibiti vitendo hivi jitihada zetu zitakuwa ni Bure kwani Hali sio nzuri," amesema.

Amewataka madiwani kushirikiana katika vita hiyo ili kuwaokoa vijana wanaofanya uhuni mitaani kwa lengo la kujipatia kipato.