Nandy: Kaeni mkao wa kula, ni mfululizo wa ngoma kali

Nandy: Kaeni mkao wa kula, ni mfululizo wa ngoma kali

Muktasari:

“Ndiyo kama naanza upya, Mungu anisaidie na mashabiki wangu endeleeni kusapoti kazi zangu”

“Ndiyo kama naanza upya, Mungu anisaidie na mashabiki wangu endeleeni kusapoti kazi zangu”

Hiyo ni kauli ya msanii Faustina Mfinanga, maarufu Nandy, alipokuwa akizungumzia ushindi wa tuzo ya Afrimma.

Anasema kila anapopata mafanikio katika muziki, ndiyo anazidi kuumiza kichwa afanye nini ili asonge mbele zaidi.

“Tuzo hii inanifanya nianze upya, huu ndiyo utaratibu wangu hata huko nyumba nilipopata nilijipanga kwa ajili ya kupata nyingine,” anasema Nandy na kuongeza.

“Siyo tuzo tu, bali hata ninapotoa muziki mzuri ukawavutia mashabiki zangu, huwa naumiza kichwa sana kufanya kazi nzuri zaidi, lengo ni kuhakikisha ninawapa nilichowaahidi na kilichonikutanisha nao ambacho ni burudani,” anasema alipokuwa katika mahojiano na gazeti hili.

Hivi karibuni msanii huyo alishinda tuzo za Afrimma zilizotolewa kwa njia ya mtandao Marekani ambapo alishinda kipengele cha msanii bora wa kike Afrika Mashariki.

Katika kipengele alichoshinda, alikuwa akichuana na wasanii kama Zuchu, Maua Sama, Rosa Ree kutoka Tanzania, Vinka wa Uganda, Akothee na Nadia Mukami kutoka Kenya.

Anasema kama kijana lengo lake ni kusonga mbele kwa mafanikio na si vinginevyo, ndiyo maana katika mambo mengi anayofanya kama binadamu muziki unachukua nafasi kubwa.

Anasema kuwa wakati huwa anatamani kubaki peke kama watu aliokaa nao hawana habari na muziki, hususani wake.

“Maisha yangu ni muziki, nauwaza nahisi na wenyewe unaniwaza, kikubwa nawawaza mashabiki zangu wanahitaji nini ndiyo maana kila siku ninafanya vitu vipya kuhakikisha siwapotezi,” anasema.

Anasema alichojifunza siku zote kila kitu kinawezekana bila kujali jinsia, rangi wala kabila.

Anakiri wasanii wa kike kuwa na changamoto nyingi hususani za kijamii, lakini hilo si sababu ya kuwarudisha nyuma.

“Tangu dunia imeumbwa hakuna historia inayoeleza mwanamke alifanikiwa tu bila kukumbana na vikwazo, hivyo ni asili na walikabiliana nayo kukiwa hakuna visaidizi na walishinda.

“Inakuwaje sisi ambao tunasaidiwa na elimu, teknolojia, asasi za kiraia na Serikali kwa kupewa kipaumbele tushindwe kuzikabili na kusonga,” anasema na kuhoji Nandy.

“Mashabiki zangu sitowaangusha, wasubiri ngoma baada ya ngoma, huku kila moja ikishindana na nyingine kwa ubora wa video na mashairi na tuzo zitakuja sana tu,” anasema.