Nani kufuata panga la Samia?

Nani kufuata panga la Samia?

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuwaweka roho juu watendaji wakuu wa Serikali yake wakiwamo mawaziri na makatibu wakuu wa wizara, akiweka wazi kwamba bado hajaweka nukta katika marekebisho anayoyafanya serikalini.


Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuwaweka roho juu watendaji wakuu wa Serikali yake wakiwamo mawaziri na makatibu wakuu wa wizara, akiweka wazi kwamba bado hajaweka nukta katika marekebisho anayoyafanya serikalini.

Alitoa kauli hiyo jana baada ya kuwaapisha mawaziri wapya wanne na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliowateua juzi.

“Hapa nilipofika kama nimeweka coma (mkato), sikuweka nukta, mabadiliko haya yanaendelea,” alisema Rais Samia kwenye hotuba yake fupi aliyoitoa Ikulu ya Chamwino, Dodoma

Mawaziri walioapishwa jana ni January Makamba (Nishati), Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi), Dk Ashatu Kijaji (Tehama) na Dk Stergomena Tax (Ulinzi). Pia alimwapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi.

Kuonyesha kwamba mabadiliko bado yanaendelea, Rais Samia wakati akimaliza hotuba yake aliwatakia kazi njema mawaziri wapya na wengine waliokuwapo kwenye hafla hiyo na kumalizia kwa kusema: “ Nami naenda kuendeleza kazi ya marekebisho.”

Suala la mabadiliko kwenye baraza la mawaziri, makatibu wakuu wa wizara na manaibu wao lilizungumzwa mara kadhaa na Rais Samia kwenye hotuba yake huku akionekana akiwafunda watendaji wapya na wale waliopo madarakani.

Alisema katika kipindi cha miezi sita cha urais wake alijaribu kuwa mkimya na mtulivu akizisoma wizara zote zinavyoendeshwa.

“Aaah, kuna mambo mengi ya kurekebisha, lakini katika kipindi hicho pia hao mawaziri, manaibu, makatibu wakuu, manaibu walinisoma mimi pia.

“Wakati mimi nawasoma wao na wao walikuwa wananisoma mimi na kama nilivyosema kati yao walichukulia ukimya na utulivu wangu, kama udhaifu na wakaanza kufanya yanayowapendeza, lakini wengine walichukulia ukimya na utulivu wangu, kama ni njia ya wao kufanya kazi na kuonyesha kwamba wanaweza kufanya kazi,” alisema Rais Samia.

Huku akionyesha kuna vitu havimfurahishi katika utendaji wa viongozi hao, alisema katika kipindi hicho cha miezi sita, alipata muda wa kutosha kujifunza, kwa sababu kabla ya hapo alikuwa makamu wa Rais na hakuwa na fursa kubwa ya kujifunza utendaji ndani ya wizara.

“Nilikuwa najifunza na nimeona sasa vipi nakwenda na nyinyi,” alisema Rais Samia huku akiongeza kuwa katika uongozi kuna mbinu mbili za kuongoza ambazo ni karoti na fimbo.

“Nami nimejichagulia njia yangu. Nataka niwaambie kwamba tunapoendelea huko, Serikali yetu itaendeshwa kwa matendo makali na siyo maneno makali. Ninaposema matendo makali wala siyo kupigana mikwaju au mijeledi, ni kwenda kwa wananchi na kutoa huduma inayotakiwa. Kila mtu kufanya wajibu wake.

“Msinitegemee kwa maumbile yangu haya, pengine na malezi yangu kukaa hapa nianze kufoka, nahisi si heshima, na kwa sababu nafanya kazi na watu wazima wanaojua jema na baya ni lipi.

Aliongeza: “Kwa hiyo ni imani yangu kwamba tunapozungumza tunaelewana na kila mtu anajua anafanya nini kwenye wajibu wake, kwa hiyo msitegemee nitaanza kufoka ovyo, kufokea watu wazima wenzangu. Nitafoka kwa kalamu.

Alisema amewaapisha mawaziri wanne na mwanasheria mmoja, lakini anafahamu kwamba wizara moja katika wizara ambazo amezipangua majukumu yake ilitakiwa uongozi wake uwepo hapa uape upya kwa sababu siyo wizara ile waliyoapia nyuma.

“Lakini, kama nilivyosema hapa nilipofika kama nimeweka koma, sikuweka nukta, mabadiliko haya yanaendelea, kwa hiyo tutakavyoendelea wizara hii nayo tutaifanyia marekebisho nao watakuja kuapa mbele yenu,” alisema.

Akizungumza kwa sauti ndogo iliyobeba ujumbe wa kuelekeza, kuonya na umakini, Rais Samia alisema mabadiliko na marekebisho anayofanya yanaendelea, kutokana na jinsi alivyoona utendaji wa mawaziri na viongozi wengine kwenye wizara zao.

Dk Mpango

Awali akizungumza kwa ajili ya kumkaribisha Samia, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, aliwataka viongozi walioapishwa wakachape kazi kwa kushikiana na wadau kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi.

“Mumuone Rais ni kama kocha anaye angalia wachezaji wake wanavyocheza na kila wakati anaitazama kama kweli inacheza na itakwenda kufunga magoli kupata ushindi. Ushindi wa Watanzania. Mkashirikiane na hao wote mnaowakuta ili matarajio ya Rais na matarajio makubwa ya Watanzania yaweze kutimia,” alisema.

Dk Mpango alimtaka Waziri Makamba (Nishati) akasimamie suala la umeme vijijini, ambako alieleza kuna kilio cha wananchi.

Pia, alimtaka waziri huyo awatupie jicho watendaji wa Tanesco, lakini vile vile aangalie maeneo ambayo hayana umeme wa gridi ya Taifa.

Kuhusu Waziri wa Ujenzi, Profesa Mbarawa, Dk Mpango alimtaka awasimamie ipasavyo makandarasi wa Wakala wa Barabara (Tanroads) na kusimamia miradi ya usafiri wa majini.

Kuhusu Dk Stergomena (Ulinzi) Makamu wa Rais alimtaka waziri huyo mpya akatumie masikio zaidi na diplomasia katika utendaji wake, hasa kwa kuwa anakwenda kufanya kazi na wanajeshi.

Pia, alimtaka Dk Feleshi aliyeapishwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusaidia kuondoa changamoto ya mikataba mibovu na kuitetea Serikali.

Spika Ndugai

Spika wa Bunge, Job Ndugai yeye alimfunda zaidi Waziri Makamba akimtaka ashughulikie suala la mradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga, aliosema kuwa kama utasimamiwa vyema utaweza kuitoa Tanzania kiuchumi.

Alimtaka pia kusimamia nishati ya gesi, iliyoonekana kusahaulika.