Nape Nnauye amchambua Rais Samia

Nape Nnauye sasa amchambua Rais Samia

Muktasari:

  • Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameanza vizuri kwa kutoa maagizo yanayoliondoa Taifa kwenye kutumia mabavu na kujielekeza kwenye kutumia akili katika ukusanyaji kodi bila kuathiri walipakodi.

Dodoma. Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameanza vizuri kwa kutoa maagizo yanayoliondoa Taifa kwenye kutumia mabavu na kujielekeza kwenye kutumia akili katika ukusanyaji kodi bila kuathiri walipakodi.

Mbali na hivyo, Nape alisema pia Rais Samia ameonyesha nia ya kuliongoza Taifa kwa kuwatendea haki Watanzania, hasa alipoitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuziangalia na ikiwezekana kuzifuta kesi zisizo na msingi wala uhalali ili kuleta haki.

Nape alisema hayo juzi kwenye mahojiano maalumu na Gazeti hili nyumbani kwake jijini Dodoma kuhusiana na Rais Samia alivyoanza kuliongoza Taifa.

Mbunge huyo wa Mtama na waziri wa zamani wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo alikuwa akizungumzia kauli ya Rais Samia ya kukataza matumizi ya kikosi kazi ‘task force’ katika kudai kodi na badala yake watumie akili na maarifa zaidi.

Sio mara ya kwanza kwa Samia kuonya matumizi ya ‘task force’ TRA, Februari 2018, wakati huo akiwa Makamu wa Rais aliwataka TRA kujenga uhusiano bora na wafanyabiashara ili walipe kodi kwa uhuru na uadilifu bila vitisho.

Pia, alionya tabia ya baadhi ya watumishi wa TRA ambao hujiunga vikundi na kuwatembelea wafanyabiashara wakijiita ‘special task force’ ambao kazi yake kubwa ni kuwatisha ili kulipa kodi.

Juzi, Rais Samia ambaye amechukua madaraka ya nchi baada ya kifo cha Rais Dk John Magufuli, alimuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba ambaye anasimamia pia TRA aache kutumia mabavu kudai kodi.

“Trend mnayokwenda nayo sasa hivi ni kuua walipa kodi. Mnatumia nguvu zaidi kuliko akili na maarifa, mnawakamua mnaenda mnachukua pesa kwa nguvu, mnazuia akaunti zao,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo, Nape ambaye aliwahi kulalamikia matumizi ya ‘task force’ bungeni, jana akizungumza na gazeti hili alisema ukusanyaji kodi ni matokeo ya utendaji mzuri wa uchumi.

Alisema kama uchumi unafanya vizuri hata ulipaji kodi utakuwa mzuri.

“Watu watalipa kodi na mtakusanya sana. Lakini, kama uchumi unafanya vibaya mnaweza mkajikuta mnabinyana sana kwa sababu watu wanafunga biashara na wakiwa wanafunga biashara, makusanyo hamuwezi mkayapata.

“Kwa hiyo mama (Rais Samia) amelizungumza hili jambo kwa weledi mkubwa, hata ukisikiliza sauti yake alikuwa anamaanisha kwamba tutumie akili badala ya kutumia nguvu katika ukusanyaji wa kodi,” alisema Nape.

Alisema suala la ukusanyaji kodi ni nyeti na kuna vyuo nchini vinavyofundisha namna ya kukusanya kodi, hata hivyo alisema haoni sababu ya kutumia watu wa pembeni kufanya kazi hiyo.

“Ni vizuri tumsaidie huyu mlipa kodi, atulipe kodi lakini aendelee kuzalisha ili na kesho alipe kodi. Huu ndio msingi mkubwa. Mama (Rais Samia) amesema vizuri sana kwamba kuna wafanyabiashara wamefunga biashara (nadhani amepewa taarifa za kutosha) hapa nchini na wamekwenda kufanya biashara nchi nyingine na wanafanya vizuri huko waliko.

“Hapa tuliwaona ni wezi, wasio wazalendo lakini wako kule wanazalisha na kule wanakozalisha wanalipa kodi, maana yake wanalipa kodi kwenye nchi nyingine na hawalipi kwetu hapa,” alisema Nape.

Nape alisema kauli ya Rais Samia itafanya uchumi upumue na kuwafanya wafanyabiashara wajisikie fahari.

“Kulipa kodi lazima iwe ni fahari, usilipe kodi huku unalia,” alisema Nape.

Pia alizungumzia wigo wa kuongeza walipa kodi kwamba kwa takwimu alizonazo, watu wanaotakiwa kulipa kodi ni karibu milioni 14, lakini wanaolipa kodi kwa sasa ni kati ya milioni 2.5 hadi milioni tatu.

“Maana yake kodi ya watu milioni 14 inabebwa na watu milioni tatu. Utaona mzigo ulivyo mkubwa hapa,” alisema Nape.

Nape Nnauye sasa amchambua Rais Samia

Kesi zisizo na msingi

Nape alizungumzia kauli ya Rais Samia ya kuwataka Takukuru kuzifuta kesi ambazo hazina msingi wala uhalali kwamba, kumekuwa na tabia ya kukamatwa na kukaa muda mrefu jela, lakini baadaye wanakuja kuachiwa huru kuwa hawakuwa na makosa.

“Kulianza kujengekea ‘trend’ na hili limejitokeza muda mrefu kidogo la kudhani kuwa tukiwa na kesi nyingi ndio mafanikio, lakini mafanikio ya kuzuia uhalifu wowote ni elimu na ushawishi mnaoutoa kwa watu.

“Idadi ya adhabu mnazozitoa ‘actually’ (kwa kweli) zinaonyesha upungufu katika namna mnavyotekeleza shughuli zenu kwa sababu kama mnatoa adhabu kwa watu ili waache vitendo vya rushwa na bado vitendo vinaongezeka na ndio maana kesi zinaongezeka. Maana yake ni kwamba hili jambo lilikuwa halifanyiki vizuri sana.

“Mama (Rais Samia) amekwenda kurekebisha, kuboresha tu kuwa hebu tusijikite kwenye idadi ya kesi, hebu tujikite kwenye kesi ambazo ni za msingi ukienda nazo zinaenda kutupa matokeo.

“Lakini, jambo kubwa kumekuwa na malalamiko ya watu kupewa kesi nyingi, wakati mwingine hata ukizisikiliza unaona wanashinda. Yaani mtu anakamatwa, anawekwa ndani anakaa muda mrefu ndani, halafu mwisho wa siku anaachiwa kuwa ameshinda yaani hana hatia.

“Unajua hata haki zake mnakuwa mmezipoteza, maana iko haja ya kufikiria namna ya kubadilisha baadhi ya sheria tuongeze wigo wa dhamana. Mtu aadhibiwe baada ya kuwa ameshapitia kwenye mchakato wa kimahakama na amekutwa na makosa,” alisema Nape.

Alisema kwa mfumo wa sasa ulivyo kuna watu wanaadhibiwa hata kabla ya mahakama haijawahukumu, kwa kesi pengine kuhisiwa.

“Unaambiwa huna kesi, lakini umeshakaa miaka, umeshasota, umeshaumia kwa hivyo nadhani wito wa mama (Rais Samia) katika masuala ya kesi ni kuzingatia haki,” alisema Nape.