Nape: Rais Samia anatosha, aachwe

Nape: Rais Samia anatosha, aachwe

Muktasari:

  • Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema Samia Suluhu Hassan ni Rais wa sita ambaye ana uwezo wa kushika nafasi hiyo hadi mwaka 2030 kama afya itamruhusu na yeye kuridhia.

Dodoma. Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema Samia Suluhu Hassan ni Rais wa sita ambaye ana uwezo wa kushika nafasi hiyo hadi mwaka 2030 kama afya itamruhusu na yeye kuridhia.

Nape, ambaye ni waziri wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipofanya mahojiano maalumu na Gazeti la Mwananchi jijini hapa.

Yafuatayo ni mahojiano hayo:

Swali; Rais Samia Suluhu Hassan amewaonya wana-CCM walioelekeza nguvu zao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Hii unalizungumziaje?

Jibu: Ni vizuri tukatafsiri hili suala la awamu kwa sababu msingi wa hili jambo ni hili suala la awamu. Kwangu kwa tafsiri ya Katiba ya CCM na tafsiri ya Katiba ya nchi. Namchukulia mheshimiwa Samia kama Rais wa awamu ya sita. Kwa sababu tulikuwa na Rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Nyerere alikaa kwa zaidi ya miaka 20 na bado tukaiita ni awamu moja.

Akaja Mzee Mwinyi (Alhaji Ali Hassan Mwinyi) tukaita awamu ya pili na alikaa miaka 10, akaja marehemu Mzee Mkapa (Benjamin Mkapa) naye tukaita awamu ya tatu, akaja Rais Kikwete (Jakaya Kikwete) akakaa miaka 10 nayo tukaiita awamu ya nne. Na hii ya marehemu Dk Magufuli (John Magufuli) na yenyewe ni awamu ya tano ambayo yeye amekaa miaka mitano na miezi kadhaa.

Kwa hiyo hii awamu iliyoanza ya Rais Samia, kwangu ni awamu ya sita. Sasa katika tafsiri ya Katiba ya CCM na hata katiba ya nchi inamruhusu mtu mmoja anayekuwa Rais kukaa kipindi cha miaka 10, kwamba anakaa mitano na anaweza kuchaguliwa tena kwa kipindi kingine na baada ya pale sasa ndio panafikia ukomo.

Kwa hiyo kwangu ni jambo ambalo ‘automatic’ (moja kwa moja) kwamba Rais Samia ameanza hii miaka minne na kitu ambayo amechukua, akimaliza kwa chama changu nadhani automatically, tutafuata tu mchakato wa kumpitisha kwenye vikao tunampa miaka mitano mingine kwa sababu anaruhusiwa kwa mujibu wa katiba kwenda kipindi kingine. Kwa hiyo ni awamu ya sita ambayo nayo tunategemea itakuwa na miaka kadhaa kwa hiyo kwetu sisi awamu sio miaka kumi kumi, awamu ni kipindi cha Rais aliyepo.

Kwa hiyo, ninadhani kwamba kwanza amefanya vizuri kuwakumbusha wakajikita kufanya kazi badala ya kuwaza 2025 na nadhani watu waliishaanza kuwaza kwa sababu walijua Rais Magufuli angemaliza 2025 akaondoka.

Sasa ni kutukumbusha tu kuwa mawazo hayo kwa sasa yanabadilika kwa sababu hatuendi tena na Rais Magufuli mpaka 2025, tunakwenda na mama Samia ambaye sasa ameanza katikati, kwa hiyo nadhani sasa mama Samia atakwenda mpaka 2030. Ili awe amemaliza awamu yake kama Mungu atampa uzima, akampa afya na yeye mwenyewe akawa yuko tayari kuendelea na kazi aliyopewa.

Lakini, kwa maana ya mifumo na mimi ningewaomba wanasiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi na hata nje ya Chama tumuunge mkono Mama Samia amalize hii miaka yake ya kwanza halafu kama afya ipo na uzima tumpe amalize na awamu nyingine ya pili, ambapo ndio atakuwa amekamilisha sasa awamu ya miaka yake 10.

Kwa hiyo tumuunge mkono na mimi ningetoa wito tusimsumbue na hata kama kuna watu waliishaanza tamaa ya 2025, hebu waache na tumpeni fursa mama afanye kazi kwa uhuru.

Afanye kazi mpaka 2025, mwaka huo tufuate mchakato ndani ya chama wa kikatiba na Katiba ya nchi tumpe tena miaka mingine na nina matumaini mama atafanya vizuri, bila shaka Watanzania watampa fursa ya kuendelea.


Kutenda haki kwa watu

Swali: Ni jambo gani ukikutana na Rais Samia utamshauri?

Jibu: Kikubwa sana nitamuambia tusimamie haki za watu, watu wasionewe, watu wasinyanyaswe, watu waone kuwepo kwenye nchi yao ni fahari. Biblia inasema haki inainua Taifa. Taifa lolote likitaka liinuke vizuri lisimamie haki.

Haki ikiwepo watu watapendana, haki ikiwemo watu wataipenda nchi yao, haki ikiwepo watapenda Serikali yao. Haki ikiwepo kutakuwa na ustawi, haki ikiwepo biashara zitashamiri, kama kuna neno moja kubwa kuliko ambalo naweza kulisema ni haki mahakamani zitendeke. Huko kwenye makusanyo ya kodi haki itendeke, kwenye mahakama haki itendeke, kwenye siasa haki itendeke, kwenye elimu haki itendeke.

Kwenye taasisi nyingine haki itendeke. Tukisimamia haki ndio ikawa ndio msingi wetu wa asubuhi, mchana hadi jioni, haki kwa kila jambo.

Sisemi kwamba hakukuwa na haki kabisa, lakini kadiri nchi inavyokua, uchumi unavyokuwa, idadi ya watu inavyo ongezeka, kunakuwa na wakati mwingine na ushawishi wa kufumbia macho haki za watu. Na yeye amesema macho yake yanaona.

Sasa afungue macho huko watu wapate haki yao, ardhi wapate haki yao, wafugaji wapate haki yao, wakulima wapate haki.

Kila mtu akipata haki yake hata hii dhana ya kazi, nifanye kazi nipate haki yangu wafanyakazi wapate haki zao, ikiwa kupewa maslahi yao wapate, wanaotakiwa kupata mishahara mizuri wapate, kila mtu apate haki. Na pale tunapobanabana hatukuweza kufikia tuwaeleze kwa nini hatukufikia.


Mabadiliko aliyoyafanya

Swali: Rais Samia ameanza kufanya mabadiliko kwenye Serikali. Una maoni gani kuhusu hilo ukilinganisha na hali ya kisiasa nchini.

Jibu: Tafsiri yangu ni kwamba Mama Samia ni zawadi ya Mungu kwa Watanzania. Amekuja kutufariji wakati wa msiba, lakini pia ataendelea kutufariji kwa kufanya mambo ambayo kwa kweli yatakuwa ni mema kwa nchi yetu.

Mama Samia ni mwanasiasa mzuri, tofauti na mtangulizi wake (Rais Magufuli) na aliwahi kukiri mara kadhaa kwamba yeye sio mwanasiasa. Lakini, Mama Samia ni mwanasiasa. Na mwanasiasa mzuri ni yule anayejua kufanya uamuzi sahihi, mahali sahihi, wakati sahihi na mtu sahihi, hii ndio tafsiri ya mwanasiasa mzuri.

Mama Samia anao huo uwezo kwa hiyo hata maamuzi anayoyafanya ukiangalia anapiga hesabu sana za kisiasa ndio maana kila akifanya watu wanamuunga mkono.

Lakini, kwa mwanasiasa yeyote mjanja akiangalia anajua mama hapa amepiga hesabu nzuri za kisiasa na nimnukuu aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Mama Margaret Thatcher, aliwahi kusema ukitaka jambo lisemwe la kisiasa mpe mwanamume, lakini ukitaka jambo litendwe vizuri mpe mwanamke.

Kwa hiyo, kwa mama hili ninampongeza kwa ujumla kwa maamuzi haya ambayo anayafanya na sina shaka kwamba, atatupa mwelekeo mpya pamoja na kuendeleza yale mambo mengi mema mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake.

Kwenye suala la kisiasa ziko hatua ambazo najua mama atazichukua na mimi nadhani tumpe muda, ameanza kuchukua ndani ya Serikali na mwezi huu mwishoni nadhani tutamkabidhi chama pia awe mwenyekiti wa chama chetu, mwanamke wa kwanza kuwa mwenyekiti katika historia.

Ninaamini pia atachukua hatua ndani ya chama na hatua hizi mbili ndani ya Serikali na ndani ya chama zitabadilisha mwelekeo wa kisiasa katika nchi yetu, ni matumaini yangu kwamba kutakuwa na uwanja mpana wa kupumua zaidi, kutakuwa na uwanja mpana wa kufanya siasa hizo.

Nape Nnauye sasa amchambua Rais Samia

Migogoro ya wizarani

Swali: Rais Samia ameonya kuhusu kudharauliana kati ya mawaziri na naibu mawaziri. Unalizunguaje hili kama waziri wa zamani?

Jibu: Wakati mwingine kama mtu hajiamini sana ndio hapo mtu anapata ushawishi wa kuanza kuhujumiana. Na kwa sababu yeye (Samia) amekuwa waziri anajua, haya mambo yanatokea kati ya waziri na naibu waziri. Waziri na katibu mkuu na mifano ipo.

Nadhani mama ameamua kuzungumzia jambo kubwa sana, kwa sababu, moja ya mambo yaliyokuwa yanatusumbua kwenye wizara nyingi ni kwamba, panapotokea mgogoro kati ya waziri na naibu waziri au waziri na katibu mkuu au watendaji wakubwa ndani ya wizara, wanabaki wanahangaika na migogoro, inachukua muda mrefu sana kuhangaika nayo badala ya kuwatumikia watu.

Na hata baadhi ya maamuzi yanashindikana kwa sababu tu jambo lako umelipeleka kwa katibu mkuu na waziri hakubaliani naye.

Ikifikia mahali watu wanaendeleza migogoro, kweli ni bora wakapumzike, wakafanye migogoro yao huko barabarani badala ya kutumia muda wa umma kufanya migogoro, watumie muda wa umma waliopewa kuwatumikia watu.

Pengine mama awe mkali katika hili ili tuweze kupata huduma iliyo bora zaidi. Sijawahi kuli-exprience, nilikaa wizarani kwa miaka kama miwili.

Labda moja ya sababu pengine naibu waziri wangu alikuwa mama mkwe wangu, kwa hiyo tulikuwa tunakaa kwa kuheshimiwa, lakini nilipofika wizarani nilikuta hii maneno kwamba bwana wenzako hapa kulikuwa na wenzako. Uamuzi huu ulishindikana kwa sababu katibu mkuu alifanya hivi.

Unaisoma kwenye mafaili unauliza uamuzi huu kwa nini haukufanyika unaambiwa kwa sababu waziri na naibu waziri walikuwa hawaelewani, uamuzi huu haukufanyika unaambiwa hili jambo liliibuliwa na naibu waziri na waziri wake hakulitaka.

Swali: Kuna wakati Rais Samia aliwahi kusema kuwa, “aliyesimama hapa ni Rais. Aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano. Unadhani ni kwa nini alitamka maneno hayo?

Jibu: Kwa maoni yangu alisema hivyo kueleza kuwa kweli Rais tuliyekuwa naye ameondoka, lakini kwa sasa tunaye Rais sio kwamba hakuna mtu wa kuongoza nchi, tunaye Rais na mambo yote sasa yaende kama yalivyo. Hata wale waliokuwa na shaka, iondoke.

Unajua kumfanya Samia kuwa Makamu wa Rais haukuwa uamuzi rahisi sana, wakati ule kwa nchi jambo hili lilikuwa halijazoeleka hata kwa chama chetu, lakini tukasema safari hii tunataka mwanamke.

Na Rais Magufuli palikuwa na mjadala wa nani apewe. Tumchukue mama au tumchukue Hussein Mwinyi au tumchukue nani.

Lakini baadaye tukasema mama anatosha, mama akapewa na maana yake ni kwamba kwa tafsiri ya katiba yetu tulikuwa tuko tayari kuwa na Rais mwanamke.

Kwa hiyo sisi viongozi tuliona tuko tayari kuwa na Rais mwanamke na huyu sasa aanze na umakamu hapa.

Sasa Mwenyezi Mungu ameamua imetokea yeye ndiyo Rais tena yuko imara kwelikweli. Kwa hiyo nadhani alikuwa anatukumbusha ni Rais amekalia kiti.