Nauli ya boti Zanzibar yapaa

Thursday May 19 2022
boti pic
By Bakari Kiango
By Jesse Mikofu

Dar/Unguja. Gharama za maisha, mafuta, vipuri na mfumuko wa bei ni miongoni sababu zilizosababisha kupanda kwa nauli ya boti za mwendokasi kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam.
Kwa sasa abiria anayesafiria kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam au Dar es Salaam kwenda Unguja atalazimika kulipia Sh 30,000 kwa daraja la kawaida badala ya Sh25,000 bei ya zamani iliyodumu kati ya miaka saba hadi minane  licha ya mafuta kupanda na kushuka.
Ongezeko la nauli hiyo, limeanza kutumika leo Mei 19 baada ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kuridhia mchakato huo.
Hata hivyo, abiria wanaotumia usafiri huo wamelalamikia hatua hiyo wakisema itawaumiza kulingana na hali ya uchumi.
Hatua ya ZMA imekuja baada ya Mei Mosi mwaka huu, Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra), kutangaza ongezeko la viwango vipya vya nauli za mabasi yanayofanya safari zake za masafa marefu na mafupi
Kwa mujibu wa Latra, kwa kilomita 30 nauli itakuwa Sh850 badala ya Sh750 kwa kilomita 35 nauli itakuwa Sh1,000 na kwa kilomita 40 nauli itakuwa Sh1,100. Wakati kwa mabasi ya mkoani daraja la kawaida kila abiria atalipa Sh41.29 kutoka Sh39.89.
Mkurugenzi mkuu wa Latra, Gilliad Ngewe alisema daraja la kati, abiria anatozwa Sh56.88 kwa kila kilomita moja badala ya Sh53.22, kiwango hicho kilichoongezwa ni Sh3.66 sawa na asilimia 6.88.
Jana Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa ZMA, Makame Sheha Ussi alisema gharama za maisha, bei za mafuta, vipuri na mfuko wa bei wa bidhaa mbalimbali ni miongoni mwa sababu za ongezeko la nauli hiyo kwa sasa.
“Hatujakurupuka kufanya uamuzi huu, tulikaa na wadau wakiwemo wataalamu na wenye kampuni hizi tuliangalia mwenendo mashine zinavyofanya kazi wake na tukapiga mahesababu. Mfano hii boti ya mwendokasi kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam kwa safari moja inatumia mafuta lita 4000.
“Mafuta wanayayoyatumia yanafanana ana dizeli, utaona namna gharama za uendeshaji zilivyokuwa kubwa. Tulikutana kwenye vikao karibu mara nne kwa nyakati tofauti na tuliangalia mambo mengi ikiwemo hawa wawekezaji ili kuhakikisha hawasitishi shughuli zao,” amesema Ussi.
Taarifa ya mabadiliko hayo yaliyoridhiwa na ZMA, ilianza kusambaa juzi  ikionesha ongezeko la bei hiyo hasa kwa daraja kati kutoka Sh25,000 hadi Sh 30,000  huku ikisema hatua imetokana kuongezeka kwa gharama za uendeshaji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ilieleza kuwa hatua hiyo imefikiwa na kampuni za usafirishaji za Azam Marine Co Ltd na Zan Fast Ferries Co Ltd waliomba kupandisha bei kwa sababu za uendeshaji.
Baadhi ya abiria waliozungumza na Mwananchi leo kwa nyakati tofauti katika bandari ya Malindi Mjini Unguja walisema hali hiyo inawaweka katika wakati mgumu kutokana na kupanda kwa gharama za maisha
Katika abiria hao wapo waliofika katika bandari hiyo kwa ajili ya kukata tiketi kutoka Zanzibar kweda Dare es Salaam lakini walishindwa kusafiri baada ya kuambiwa nauli za boti zimependa.
“Nimefika hapa nimeambia bei imepanda tena ghafla ipo juu, nimeshindwa kusafiri maana sikuwa na fedha nyingine hadi nijipange tena kwa sbabu nilikuwa na matatizo,” amesema Halima Said.
Abiria mwingine Samwel Simon amesema upandishaji wa bei za usafiri wa boti utaathiri abiria wengi maana gharama za maisha zimepanda na kila kitu kimekuwa uchumi wake umekuwa.

Advertisement