NCCR-Mageuzi wamvua uongozi katibu mkuu

Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma Chama cha NCCR Mageuzi, Edward Simbeye akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maazimio ya kikao cha Halmashauri  Kuu ya NCCR Mageuzi Taifa, kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, upande unaomuunga mkono, James Mbatia iliyojifungia kwa siku moja umeazimia 14 ikiwemo kumvua uongozi katibu mkuu wao Martha Chiomba

Dar es Salaam. Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, upande unaomuunga mkono, James Mbatia iliyojifungia kwa siku moja imeazimia kumvua uongozi katibu mkuu wa chama hicho, Martha Chiomba.

Pia, kikao hicho kilichofanyika jana Jumamosi Agosti 13,2022 kiliazimia pia  Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Zanzibar Haji Ambari Khamis kuchukuliwa hatua za kinidhamu ndani na nje ya chama kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania wakidai kuwa kiongozi huyo anadaiwa kusababisha vurugu ndani ya NCCR-Mageuzi kwa kutumia vibaya nafasi yake.

Hata hivyo, alipotafutwa Chiomba kuzungumzia uamuzi huo, amesema kesho atazungumza na wanahabari katika ofisi za makao ya chama hicho, Ilala Dar e Salaam.

Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Edward Simbeye amewaambia waandishi wa habari leo Jumapili Agosti 14, 2022 kwamba kikao kilihudhuriwa na wajumbe 47 kati ya 81, akisema kwa mujibu wa utaratibu akidi ya kikao hicho ilitimia. Amesema katika kikao hicho wameazimia masuala 14.

“Kikao kimeazimia kumvua nafasi ya uongozi Chiomba na nafasi yake itakaiminiwa na naibu katibu mkuu Bara kwa mujibu wa katiba,” amesema Simbeye.

Mbali na hilo, wajumbe hao wameazimia kuteua kamati maalumu iliyokasimishwa majukumu ya kuanza kushughulikia tuhuma zinazowahusu viongozi wao akiwamo, Haji Ambar Khamis, Chiomba, Ameir Mshindani, Susan Masele na wajumbe wote waliosababisha mgogoro ndani ya chama hicho.