Nchi 60 kushiriki tamasha la kimataifa Bagamoyo

Nchi 60 kushiriki tamasha la kimataifa Bagamoyo

Muktasari:

  • Nchi 60 zinatarajiwa kushiriki tamasha la kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo litakalofanyika  kuanzia Oktoba 28 hadi 30 katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo(TaSUba).

Pwani. Nchi 60 zinatarajiwa kushiriki tamasha la kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo litakalofanyika  kuanzia Oktoba 28 hadi 30 katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo(TaSUba),wilayani Bagamoyo

Hayo yamesemwa leo Jumapili Oktoba 17, 2021 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TaSUba, Dk Herbert Makoye kwenye mkutano wa waandishi wa habari kuhusu tamasha hilo.

Dk Makoye amesema tamasha hilo ambalo ni la 40 kufanyika, kwa mwaka huu jumla ya washiriki kutoka nchi 60 wamethibitisha kushiriki.

"Tunatarajia kupokea ugeni kutoka nchi 60 na tayari maandalizi ya tamasha hilo yapo vizuri mpaka sasa," amesema.

Dk Makoye alitaja moja ya malengo ya kufanyika kwa tamasha hilo kuwa ni pamoja na kuenzi na kutunza utamaduni.

Faida nyingine ni wanafunzi wanaosoma chuoni hapo kuonyesha kwa vitendo nini walichojifunza darasani.

Pia ni jukwaa  la wasanii kukutana na wasanii wa ndani na nje ya nchi kubadilishana uzoefu na kujenga mawasiliano na kubwa kuliko kutoa burudani kwa Watanzania na wageni.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Abdallah amesema wao kama wasaidizi wa Rais Samia Suluhu Hassan wameamua kuendeleza na kumuunga mkono katika jitihada zake za kutangaza utamaduni wa Tanzania.

"Kama mlivyoona  ni siku za karibuni Rais wetu alifanya ziara ya Royal Tour katika kutangaza utamaduni, sanaa na vivutio vyetu, hivyo tamasha hili ni katika kuendelea kumuunga mkono katika hilo na kuiweka Bagamoyo katika ramani dunia iijue," amesema Zainabu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa(Basata), Matiko Mniko amesema watahakikisha wadau wao wote wanashiriki katika tamasha hilo wakiwemo wasanii wa singeli, dansi, injili  na sanaa za maonyesho.

Wakati Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Dk Kiagho Kilonzo amesema watatumia tamasha hilo pia kuonyesha filamu ambazo zinashindanishwa katika tuzo za filamu mwaka huu ambazo ni kwa mara ya kwanza Serikali inazisimamia.

"Katika siku zote hizi tatu za tamasha tutakuwa na hema lenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 100 kwa ajili ya kuonyesha filamu mbalimbali, ambazo kati ya hizo ni zile zinazoshindanishwa kwenye tuzo,"alisema Dk Kilonzo.