Ndugai akerwa wabunge kuitwa mazuzu

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Muktasari:

  • Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema anakerwa na tabia ya baadhi ya watu kuwaita wabunge mazuzu na kuwataka wajenge utamaduni wa kuheshimiana.


Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema anakerwa na tabia ya baadhi ya watu kuwaita wabunge mazuzu na kuwataka wajenge utamaduni wa kuheshimiana.

Akifungua wiki ya Azaki jijini Dodoma leo Jumamosi Oktoba 23, Ndugai amesema, “Sio unaitwa Azaki basi unawasema wenzako maneno unayotaka ya hovyo. Tumewahi kugombana na baadhi ya wazee, mzee unatuita jina sisi hatulipendi…Hivi tumekosea wapi kama unamuita mtu jina la Juma anasema mimi jina hilo silitaki.

“Tatizo lako nini? Unang’anga’ania kuita hilo jina, we ni nani? Haiwezekani kama mwanadamu akikwambia hiki sina raha nacho kiache na wewe hukiachi, kama kweli wewe ni muungwana mtu wa Mungu utakiacha.”

Amesema matokeo ya kutoheshimiana ni wazee (ambao hakuwataja) wanawasema wabunge ni mazuzu wakati wana akili.

Amesema wao hawana muda wa kubishana bishana na watu wana namna hiyo.

Amesema yeye amechaguliwa na watu 400,000 kuwa mbunge kwa miaka 25 katika chaguzi mbalimbali na tena mara mbili amepita bila kupingwa.

“Hata kesho nikienda kusimama (kugombea) tafuta wa kusimama na mimi hutampata. Akisimama ni mpambe wa kusindikiza. Halafu wewe unaniita zuzu yaani wale watu una maanisha ni mazuzu wamechagua zuzu mwenzao?”amehoji.

Ndugai alipongeza Azaki kwa kazi nzuri wanazofanya lakini akasema wachache wao wamekuwa wakitumika na wana ajenda zisizokuwa za kwao na kwamba Azaki chache zimekuwa na ajenda za kupata fedha kutoka mahali fulani (hakukutaja).

“Sasa kama we njaa yako ni hela ndio maana lazima zitungwe sheria sasa zinazokufuata kwenye hela. Eeeeh utatuambia nani amekupa, kiasi gani, ziko wapi, utazitumiaje na utaleta taarifa kwa kila shilingi zamani haikuwa hivyo tuliaminiana lakini baada ya kuona mwenendo usio ridhisha ndio tukatunga sheria,”amesema.

Ndugai amesema kama wasipoweka sera ya kuambiana na kurekebishana (wao kwa wao mashirika) basi hata sheria zitakazotungwa siku za usoni zitakuwa kali zaidi.