Ndugu wa anayedaiwa kujinyonga wajitokeza

Muktasari:

  • Ndugu wa marehemu Gaston Moshi (25) anayedaiwa kujinyonga katika Kituo cha Polisi Bonanza jijini Dodoma na mwili wake kukaa mochwari kwa siku 14, wameziomba mamlaka husika kufanya uchunguzi kuhusu sababu za kifo cha jamaa yao.


Dar es Salaam. Ndugu wa marehemu Gaston Moshi (25) anayedaiwa kujinyonga katika Kituo cha Polisi Bonanza jijini Dodoma na mwili wake kukaa mochwari kwa siku 14, wameziomba mamlaka husika kufanya uchunguzi kuhusu sababu za kifo cha jamaa yao.

Mwili wa Moshi ulikaa chumba cha kuhifadhia maiti kwa siku 14 katika Hospitali ya General jijini hapa, baada ya ndugu wa marehemu kutokuwa na taarifa ya kifo chake hadi waliposoma katika gazeti hili.

Mwananchi kwenye toleo la Septemba 17 na 19, mwaka huu na mitandao yake lilikuwa an habari inayoeleza mwili wa Moshi kukaa mochwari kutokana na ndugu zake kutojitokeza.

Akizungumza katika Ofisi za Mwananchi jijini Dodoma jana, kaka wa marehemu, Paul Habib alisema anashangazwa na kilichomkuta ndugu yao. “Hakuwa na makuu mlevi wa pombe wala wanawake, kwa nini wamemtesa hivi siku 14 mochwari hapana hapana inaumiza sana,”alisema Habib.

Alisema walipokwenda hospitali kuuangalia mwili wake waliukuta na jeraha kubwa la kupasuka mdomoni na nguo zake zilikuwa na damu iliyoganda. “Ni kama mtu aliyepigwa sana, tunataka uchunguzi ufanyike kubaini kama kweli ndugu yetu alijinyonga na kama ni kweli lile jeraha mdomoni limetoka wapi? maana inaonekana kapigwa na kitu kizito.

“Na baada ya kugundua amefariki kwa nini askari wasitoe taarifa ya kifo kule walipomkamata mpaka aanze kutafutwa? ”alihoji Habib.

Kwa upande wa shemeji wa marehemu, Martin Victor alisema “Ombi letu kama ndugu tunaomba haki, kuna kitu kimejificha kama alifia kituoni ni kwa nini taarifa hazijapelekwa katika eneo ambalo anafanyia kazi.

“Tunataka tujue huyo aliyeuleta mwili mochwari ni nani atueleze ndugu yetu ilikuwaje akajinyonga,”alisema.

Alisema walipata taarifa kupitia wafanyakazi wa Kampuni ya Simu ya Airtel mkoani Morogoro.

Alisema marehemu alikuwa akifanya kazi katika kampuni hiyo, hivyo walivyoiona habari katika gazeti la Mwananchi wakampigia simu mdogo wake na marehemu aitwaye Ibrahim wakimtaka afike ofsini.

“Alipofika ofisini alionyeshwa picha iliyokuwa katika gazeti na kukiri kweli ni ndugu yake na kutoa taarifa kwa mama (Ester Thomas), anayeishi Bigwa na kuitishwa kikoa cha familia kujadili”alisema

Habib alisema katika kikao hicho waliwateua watu watatu kuja Dodoma kwa ajili ya kujua ukweli wa tukio.

“Ndio nikaja mimi na Deogratous Kufaa ambaye ni mdogo wa marehemu na huyu shemeji yetu (Martin Victor).

Alisema waliingia Dodoma juzi usiku na ilibidi wasubiri mpaka asubuhi ya jana ndio walienda hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma kuangalia kama kweli ni ndugu yao na walipoonyeshwa mwili kweli alikuwa ni ndugu yao na wameuchukua kwa ajili ya mazishi.


Walishukuru Mwananchi

Habib alisema “Tulipokuwa tunakuja Dodoma, mama alisema tufike kwenye ofisi za gazeti la Mwananchi na kumshukuru aliyeandika habari hiyo na uongozi kwa ujumla,”Hatuna cha kuwalipa ila Mwenyezi Mungu, ahsanteni sana.

Kamanda ashindwa kutoa majibu

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno kuzungumzia tukio hilo alisema “Nipeni muda mchache nifuatilie, hata hivyo alipopigiwa mara kadhaa hakupokea tena simu hadi gazeti linakwenda mtamboni.