Ndugulile aagiza kuimarishwa kwa mawasiliano mipakani

Ndugulile aagiza kuimarishwa kwa mawasiliano mipakani

Muktasari:

  • Waziri wa Mawasiliano ameagiza changamoto ya mawasiliano maeneo ya mipakani imalizwe haraka ili Watanzania waishio katika maeneo hayo waondolewe hofu ya mawasiliano.

Dodoma. Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustin Ndugulile ameagiza kufanyika mageuzi ya haraka maeneo ya mipakani ili kuondoa changamoto ya mwingiliano wa mawasiliano.

Dk Ndugulile ametoa kauli hiyo leo Januari 25 jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiliaji saini mkataba wa awamu ya 5 wa kupeleka mawasiliano katika vijiji 173 nchini.

Mikataba hiyo imeingiwa baina ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kampuni za simu za Vodacom, Airtel na Tigo yakilenga kuzifikia kata 61 zenye wakazi zaidi ya 728,840.

Waziri huyo amesema ni wakati kwa Serikali kuondoa kero hiyo kwa kuwa si nzuri hata inawanyima haki  Watanzania waishio mipakani.

“Hizo changamoto mnapaswa kuziondoa kwani kumekuwa na kelele kwa watu wanaoishi mipakani ambao mitandao inakuwa na muingiliano na wenzetu wa nje,” amesema Waziri Ndugulile.

Dk Ndugulile amewaagiza wenye makampuni kuheshimu mikataba waliyotiliana ili ndani ya kipindi cha miezi 9 vijiji hivyo viwe na mawasiliano.

Amesema serikali haitamvumilia wala kumfumbia macho mtu atakayekuwa na nia ya kukwamisha mpango huo kwakuwa inatambua mawasiliano ni uti was mgongo katika uchumi.