NEC: Mafanikio maboresho daftari la wapiga kura yanahitaji ushirikiano

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Ramadhani Kailima akifungua mkutano kati ya wadau na tume hiyo wilayani Rorya. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema ili mafanikio yawepo kwenye maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura, ushirikiano wa wananchi unahitajika kwa kiasi kikubwa kuepuka watu wasio na sifa kuandikishwa.

Rorya. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema ili mafanikio yawepo kwenye maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura, ushirikiano wa wananchi unahitajika kwa kiasi kikubwa kuepuka watu wasio na sifa kuandikishwa.

Akizungumza kwenye mkutano na wadau wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara leo Jumatatu Novemba 20, 2023, Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima amesema tume hiyo imejipanga kuhakikisha kila mwenye sifa ya kuandikishwa kwenye daftari hilo anapata nafasi.

“Ndiyo zipo taasisi zinazohusika na kutambua raia na wasio raia lakini mtambuzi wa kwanza ni wewe mwananchi unapofika pale ukamkuta mtu asiyekuwa raia anajiandikisha toa taarifa lakini pia baada ya maboresho tunaleta daftari kwenye kata husika wananchi jitokezeni mkaangalie kama kuna watu walioandikishwa wakati sio raia na mtoe taarifa,”amesema

Katika mkutano huo wenye lengo la kuanza maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuanza majaribio katika Kata za Ikoma wilayani humo na Kata ya Ng’ambo Manispaa ya Tabora, Kailima amesema yapo maboresha yaliyofanywa na tume hiyo ili kurahisisha shughuli ya uboreshaji ikiwa ni pamoja na vifaa.

Ambapo amedai vifaa vya awali vilikuwa na chagamoto kadhaa ikiwemo uzito mkubwa uliopelekea usafirishaji wake kuwa mgumu.

"Kwasasa tutatumia VRS ambayo ina kishikwambi ambavyo uzito wake ni kilogram 15 wakati awali tulitumia BVR ambayo ilikuwa na uzito wa kilogram 35 na kifaa kimoja kwasasa kina uwezo wa kuandikisha watu zaidi ya 200 kwa siku na mtu mmoja anaandikishwa chini ya dakika 10,"amesema

Amedai ili kufanikisha uboreshaji huo, tume hiyo inatarajia kufanya maboresho ya majaribio katika kata hizo kuanzia Novemba 24 hadi 30 mwaka huu ili kuangalia ufanisi wa vifaa na kama kuna changamoto  zifanyiwe kazi kabla ya maboresho hayo kuanza 2024.

Wakili Mkuu wa Serikali, Rose Chilongozi amesema  tume hiyo imeandaa utaratibu wa watu wanaotaka kurekebisha taarifa zao kufanya hivyo kwa njia ya mtandao kwa taarifa za awali kabla ya kwenda kukamilisha marekebisho hayo katika vituo vya uandikishaji.

"Kwa wale wanaotaka kurekebisha taarifa zao watakuwa na uwezo wa kufanya marekebisho hayo ya awali kupitia mtandao na kisha kwenda kwenye vituo kwaajili ya ukamilishaji yaani kupiga picha na kusaini kisha kupewa kadi,”amesema

Wakitoa maoni yao, wadau wameonyesha wasiwasi wao kuhusu ufanisi wa uchaguzi mkuu ujao kwa madai kuwa uliopita uligubikwa na mambo mengi ambayo ni kinyume cha utaratibu.

"Upo uwezekano wa watu kutumia mwanya wa kuwa mpakani wakaingiza watu wasiokuwa raia wakaandikishwa na kisha kupata fursa ya kupiga kura kinyume na utaratibu,"amesema Baraka Samson

Amesema kutokana na hali hiyo ipo haja ya tume hiyo kuongeza idadi ya maofisa uhamiaji hasa katika maeneo ya mipakano ili kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kutokea wakati wa uandikishaji.

Ester Nyaonge amesema changamoto ya umbali wa vituo vya kujiandikisha inapaswa kufanyiwa kazi akidai imekuwa kikwazo kwa watu wengi wakiwemo wenye mahitaji maalum kushindwa kufika katika vituo hivyo.