Necta yasema ufaulu kidato cha nne umeongezeka

Katibu Mtendaji Baraza la Mitihani Tanzania, Charles Msonde akitoa taarifa ya matokeo ya upimaji wa darasa la nne, kidato cha pili na mtihani wa kidato cha nne na maarifa (QT) iliyofanyika mwaka jana. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Necta yatangaza matokeo ya kidato cha nne, yasema ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.46 ikilinganishwa na mwaka jana, shule ya Kemebos ya Kagera yaibuka kinara katika 10 bora kitaifa

Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde amesema jumla ya watahiniwa 483,820 sawa na asilimia 87.30 wamefaulu mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2021.

Dk Msonde ameibainisha hayo leo Jumamosi Januari 15, 2022 wakati akitangaza matokeo ya darasa la nne, kidato cha pili na nne.

Amesema kati ya watahiniwa 483,820 wasichana waliofaulu 218,174 sawa na asilimia 85.77 huku wavulana wakiwa 204,214 sawa na asilimia 89.00 wamefaulu.

“Mwaka 2020 watahiniwa 373,958 sawa na asilimia 85.84 wa shule walifaulu mtihani huu. Hivyo ufaulu wa watahiniwa wa shule umeongezeka kwa asilimia1.46 ikilinganishwa na mwaka 2020,” amesema Dk Msonde.

Katika matokeo hayo, Dk Msonde amesema shule ya Kemebos ya Kagera imeshika nafasi ya kwanza katika 10 bora kitaifa ikifuatiwa na shule za St. Francis (Mbeya),  Waja (Geita), Bright Future Girls (Dar es Salaam) Bethel  Sabs Girls (Iringa), Mau Seminary (Kilimanjaro) na Feza Boys’ (Dar es Salaam).

Shule nyingine ni Precious Blood ya mkoa wa Pwani, Feza Girls’ (Dar es Salaam) na Mzumbe ya mkoani Morogoro.

Dk Msonde amesema Consolata Lubuva aliyekuwa akisoma St Francis ameibuka wa kwanza kitaifa katika orodha ya 10 bora ya watahiniwa waliofanya vizuri.