Netanyahu, Prince Mohammed wakutana kisiri Saudi Arabia

Monday November 23 2020
NETANYAHU PIC

Netanyahu, Prince Mohammed
wakutana kisiri Saudi Arabia


Summary: Kumekuwepo na ubashiri ulioenea nchini Israel na Marekani, kuwa taifa hilo kubwa duniani linasukuma nchi nyingi za Kiarabu kuingia katika makubaliano na Israel, maarufu kama Abraham Accords, kabla ya rais-mteule Joe Biden hajaapishwa.

Jerusalem. (AFP)
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amefanya mazungumzo ya siri nchini Saudi Arabia pamoja na mtoto wa mfalme, Mohammed bin Salman, vyombo vya habari vimeeleza, ikiwa nui safari ya kwanza iliyoripotiwa ya waziri huyo. 
Mkutano huo, ulioripotiwa leo na shirika la utangazaji la Israel la Kan na mashirika mengine, umekuja wiki kadhaa baada ya taifa hilo la Uyahudi kufikia makubaliano ya kihistoria kusawazisha mambo na washirika wawili wa Saudi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain.
Hata hivyo, Saudi Arabia imekanusha habari hizo za vyombo vya habari vya Israel kuwa kulikuwa na mazungumzo kati ya Prince Mohamed na Netanyahu wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo.
"Nimeona ripoti za vyombo vya habari kuhusu mkutano kati ya Prince HRH na viongozi wa Israeli wakati wa ziara ya @SecPompeo," alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi, Prince Faisal bin Farhan katika akaunti ya Twitter.
"Hakuna mkutano kama huo uliofanyika. Maofisa pekee waliokuwepo ni kutoka Marekani na Saudi."
Hata hivyo, ripoti hizo zinasema makubaliano hayo, yanayojulikana kama Abraham Accords, yalifikiwa na uongozi wa Rais Donald Trump, ambaye anaondoka marakani katika kipindi kisichozidi miezi miwili.
Kumekuwepo na ubashiri ulioenea, nchini Israel na Marekani, kuwa taifa hilo kubwa duniani linasukuma nchi nyingine kuingia katika makubaliano ya Abraham Accords kabla ya rais-mteule Joe Biden hajaapishwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, ambaye alikuwa Israel wiki iliyopita, pia alikuwemo katika mazungumzo hayo yaliyoripotiwa, kwa mujibu wa mwandishi wa masuala ya diplomasia wa Kan. 
Pompeo amethibitisha kuwa alikuwa Neom kama sehemu ya ziara ya Mashariki ya kati na alikutana na Prince Mohammed, ambaye anajulikana zaidi kwa vifupisho vya majina yake, MBS.
Hadharani, Saudi Arabia imesema itaendelea na msimamo wake wa miaka mingi wa nchi za Kiarabu wa kutokuwa na uhusiano na Israel hadi mgogoro baina ya taifa hilo la Kiyahudi na Palestina utakapotatuliwa.
Wapalestina wamelaumu makubaliano hayo ya Abraham Accords wakiyaita ya "kuchomwa kisu mgongoni", na kushauri mataifa ya Kiarabu kuendelea na msimamo hadi Israel itakapoachilia ardhi inayoikalia ya Palestina na kukubali kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

Advertisement