Ngoma nzito Bunge lijalo la Kenya

Ngoma nzito Bunge lijalo la Kenya

Muktasari:

Burhan alikiri kuwepo kwa tatizo hilo, lakini akasema halitokani na mashine zao kuharibika.

Nairobi. Zikiwa zimepita siku tano tangu Uchaguzi Mkuu nchini Kenya, ufanyike Agosti 22, 2022 huku nafasi mbalimbali zikiwaniwa, zikiwemo urais, ugavana, ubunge na udiwani, mchuano mkali kati ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza, sasa umehamia kwenye Bunge.

Nafasi ya urais ndiyo yenye ushindani mkali kati ya Naibu Rais William Ruto ambaye hadi sasa inaonekana anaongoza kwa kupata kura milioni 6.7, akifuatiwa na Raila Odinga wa Azimio la Umoja mwenye kura milioni 6.6 na wafuasi wa kambi hizo mbili kila mmoja anajinasibu kushinda.

Hali ya ushindani imeendelea hadi kwenye wawakilishi wa wananchi watakaoingia kwenye nyumba ya maamuzi (Bunge), huku kambi hizo mbili zimeendelea kuchuana kwa karibu na kutabiriwa Bunge lijalo linaweza kuwa na idadi inayokaribiana ya wabunge kwenye Bunge lenye wabunge 349.

Mpambano huo mkali unaonyesha dalili ya kuwepo kwa ugumu wa kupitisha mambo kwa Serikali itakayokuwa madarakani, hasa wakati wa bajeti na miswada ya sheria mbalimbali.

Abdul Jamal, mchambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa, ameliambia Mwananchi kuwa kukaribiana huko kwa wawakilishi kutaulazimisha upande mmoja usiwe na uwezo wa kupeleka hoja na kuamua bila kushawishi upande mwingine utakaounga mkono hoja husika.

“Siasa za Kiafrika za wabunge wa upinzani kupinga mambo mengi yanayoletwa na Serikali bungeni naona Bunge lijalo la Kenya litakuwa na changamoto hiyo, ingawa ni nzuri kwa kuwa itaifanya Serikali kuwa makini na kila inachokifanya,” alisema.

Alisema upinzani unapokuwa mkali ndani na nje ya Bunge ndivyo huduma mbalimbali zinaboreka kwa kuwa kila upande utataka ufanye mambo kwa umakini.

“Tumeshuhudia mara kadhaa wabunge wa upinzani nchini Tanzania wakitoka bungeni kubishia maamuzi fulani, lakini pia tumekuwa tukiona kura za wazi za kupitisha bajeti ambazo wabunge wa upinzani mara zote kura yao hukataa kuipitisha bajeti, lakini bahati nzuri CCM ina wabunge wengi hupita, hiki sikioni kwa Kenya,” alisema

Hata hivyo, pia kuna dalili kuwa Bunge lijalo la Kenya linaweza kuwa na idadi ya wabunge wa chama ambacho rais hatashinda (upinzani), hali ambayo inaweza kuathiri baadhi ya uendeshaji wake, hasa katika maamuzi, ikizingatiwa ili jambo lipitishwe na Bunge la Kenya, kanuni zinaonyesha ni lazima theluthi mbili wabunge walikubali.


Hali ilivyo

Kati ya wabunge 349, mbili ya tatu ni sawa na wabunge 232 ambayo ni sawa na asilimia 67% ya wabunge wote wanaopatikana kwa njia kuu tatu ambapo 290 wanachaguliwa moja kwa moja kutoka kwenye majimbo yao, wabunge 47 ni wanawake ambao wanatoka kwenye kila kaunti na wabunge 12 kutoka kwenye makundi maalumu.

Mpaka jana saa 7 mchana, mgombea mwenza wa tiketi Azimio la Umoja, Martha Karua akiwa kwenye sherehe na viongozi waliochaguliwa kupitia muungano huo, alisema mpaka muda huo walikuwa wameshinda viti 180 vya ubunge, huku mshindani wao Kenya Kwanza akipata viti 130.

Hata hivyo mpaka muda huo matokeo yote ya nafasi za ubunge bado yalikuwa hayajatangazwa katika baadhi ya maeneo, ikiwemo Mombasa. Uchaguzi wao mdogo utafanyika leo kutokana na kuwepo kwa sababu mbalimbali zilizopelekea kuahirishwa Agosti 9, 2022.

Kabla ya Karua kutoa kauli hiyo, mgombea urais wa tiketi ya Kenya Kwanza, William Ruto alituma ujumbe wa kuwaongeza washindi wa nafasi mbalimbali kutoka kambi yake ya Kenya Kwanza, huku pongezi za pekee akizitoa kwa washindi wanawake.

“Kwa upekee niwapongeze wanawake walioshinda kwenye nafasi mbalimbali kwa kuweza kushinda vikwazo na kuipanda ngazi ya siasa, kila la heri kwenye utekelezaji wenu wa majukumu mapya, wahangaikaji tupo pamoja na nyinyi,” alisema.

Ukiachana na Bunge hilo la wabunge wa majimbo, lakini pia Kenya kuna Bunge la seneti ambalo linaundwa na viti 67, huku mpaka sasa mchuano ni mkali kati ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza.

Kenya Kwanza wameonekana kuwa na idadi kubwa ya wabunge wa seneti, ikiwa na maseneta 24 ikilinganishwa na 23 walioshinda kutoka Azimio la Umoja.

Kenya Kwanza wameshinda viti vyote vya nafasi ya ubunge kutoka kwenye ukanda wa Mlima Kenya ambao pia anatokea Rais Uhuru Kenyatta, anayemuunga mkono Odinga.

“Sasa ni rasmi, Kenya Kwanza ina idadi kubwa ya wabunge kwenye Bunge la Seneti. Asante Wakenya kwa uaminifu,” Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter.

Idadi hii ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya Jubilee iliyokuwa nayo baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2017 ilipojinyakulia viti 27 kati ya 47 vilivyopatikana na kuhakikishiwa nafasi zaidi za useneta.

Tofauti na uchaguzi uliopita, upande wa Odinga ambao pia wapo kwenye muungano wa Azimio la Umoja, nafasi za maseneta zimeongezeka ikilinganishwa na uchaguzi uliopita, huku mwaka 2017 akipata wabunge wa seneti 20, huku hadi sasa amepata 23.