Nguvu zisizime sauti za wanaodai Katiba Mpya

Nguvu zisizime sauti za wanaodai Katiba Mpya

Muktasari:

  • Ibara ya 3. (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema; “Jamhuri ya Muungano (wa Tanzania) ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa”

Ibara ya 3. (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema; “Jamhuri ya Muungano (wa Tanzania) ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa”

Kwa kuzingatia msingi huo wa Katiba, sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 ilitungwa kulinda haki za kisiasa na kutoa haki kwa vyama vya siasa kufanya shughuli za siasa kueneza sera kushawishi umma kwa lengo la kushinda chaguzi huru, na za kidemokrasia na hatimaye kuongoza dola.

Katika Ibara ya 12. (1) na 13. (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, suala la usawa mbele ya macho ya sheria unasisitizwa huku Ibara ya 13. (4) ikizipiga marufuku mamlaka yoyote nchini kutenda kwa ubaguzi iwe kwa kuangalia utaifa, kabila, dini, jinsia, itikadi za kisiasa, rangi au hali ya kiuchumi.

Nimenukuu baadhi ya Ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania ya mwaka 1977 na kutaja sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kupata mtiririko mzuri wa kujenga hoja yangu kuhusu aina ya utendaji tunaoushuhudia miongoni mwa baadhi ya viongozi na watendaji ndani ya Jeshi la Polisi nchini.

Kiuhalisia, kuna tatizo miongoni mwa baadhi ya viongozi na watendaji wa Jeshi la Polisi lililoanza tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa uliporejeshwa mwaka 1992.

Baadhi ya viongozi na watendaji wa Jeshi la Polisi bado wamesalia kwenye fikra ya ukada kwa chama tawala ambao enzi hizo ilikuwa ni moja ya sifa za ajira serikalini bila kutambua kwamba enzi zimebadilika na sasa Tanzania ni nchi yenye mfumo wa vyama vingine unaotoa fursa kwa vyama vyote kufanya siasa.

Mfano hai ni jinsi baadhi ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa wanavyoshughulikia masuala yanayohusu viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani.

Mjadala ya Katiba Mpya inayoendelea nchini kuanzia kwenye vikao na majukwaa rasmi ya kisiasa na mitandao ya kijamii ni mfano hai wa fikra za ukada kwa chama tawala kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa Jeshi hilo.

Suala la Taifa kuandika Katiba Mpya au la limegawanya watu katika makundi mawili; moja likidai Katiba huku jingine likiamini iliyopo bado inakidhi mahitaji, hivyo siyo muda mwafaka wa kuandika mpya.

Kimsingi, makundi yote mawili yana hoja ya msingi ambayo kila upande unatakiwa kusikiliza ili kutoa fursa ya kushindanisha ubora wa hoja zao.

Wanaotaka Katiba Mpya wasikilizwe hoja zao na kujibiwa kwa hoja. Vivyo hivyo wanaotetea Katiba ya sasa pia wasikilizwe na kujibiwa kwa hoja. Huo ndiyo msingi wa majadiliano katika jamii yoyote yenye watu waliostaarabika. Tanzania ikiwemo.

Hata hivyo, kuna dalili kuwa iwe kwa kuagizwa au kwa kujituma wenyewe, wapo baadhi ya viongozi na watendaji ndani ya Jeshi la Polisi wanafanya kila wanaloweza kuzima siyo tu hoja ya madai ya Katiba Mpya, bali pia hata sauti za wenye hoja hiyo.

Tumeona baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani wanaotoa hoja za kudai Katiba Mpya wakijikuta matatani kwa vikao na shughuli zao halali kuingiliwa, kutiwa mbaroni na kulazwa mahabusu.

Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa uhuru wa maoni, hivyo, siyo sahihi dola kutumika kuziba midomo ya wenye hoja kinzani na kada tawala.

Wanaotaka Katiba Mpya wanadai iliyopo imepitwa na wakati kulingana na mahitaji na maisha ya sasa, hasa ya mfumo wa vyama vingi, haki za kiraia na demokrasia kwa sababu ilitungwa wakati wa mfumo wa chama kimoja na hivyo kutokidhi muafaka wa Kitaifa wa vyama vingi.

Wanadai Taifa linahitaji Katiba Mpya inayosimamia misingi ya muafaka wa Kitaifa kulingana na mahitaji mapya ya kisiasa, mazingira mapya ya kisiasa na changamoto mpya badala ya hii ya sasa ambayo licha ya kufanyiwa marekebisho mara 14, bado haitoi fursa ya ujenzi wa Taifa bora yenye maendeleo endelevu na inayoongozwa kwa misingi ya sheria.Mwanga wa matumaini ya kupata Katiba Mpya ulianza mwaka 2010, baada ya Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete kutangazia umma nia ya Serikali ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba Mpya ikifuatiwa na kutungwa kwa sheria ya mabadiliko ya Katiba mwaka 2011.

Pamoja na mchakato wa kuandika Katiba Mpya kukwama njiani, Chama Cha Mapinduzi kiliamua kuweka suala hilo katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015 -2020 kwa kuahidi umma kuendelea na mchakato huo.

Kama Taifa, tuzingatie wosia wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete wa “Hoja haipigwi rungu; bali hujibiwa kwa hoja bora na imara zaidi” kwa kuwasikiliza kwa usawa wanaotaka Katiba Mpya na wanaopinga hoja hiyo. Mungu Ibariki Tanzania! 0766434354.