NHC kujenga nyumba 5000 kumuenzi Rais Samia

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Muungano Saguya akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Shirika hilo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 leo Agosti 09, 2022 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma.

Muktasari:

Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) limejipanga kumuenzi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga nyumba 500 za kuuza na kununua nchini kwa gharama ya Sh466 bilioni.

Dodoma. Jumla ya Sh466 bilioni zimepangwa kutumiwa na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) katika ujenzi wa nyumba za kuuza na kupangisha 5000 katika mradi unaojulikana kama Samia Housing Scheme (SHS).

Meneja Habari na Uhusiano wa shirika hilo, Muungano Saguya ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 9, 2022 wakati akielezea utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023 ya shirika hilo.

Amesema huo unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo shirika hilo linatamani Watanzania kukumbuka kwa miaka mingi ijayo.

Saguya amesema asilimia 50 ya nyumba hizo zitajengwa Dar es Salaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine asilimia 30 katika mradi huo ambao ujenzi wake utakwenda kwa awamu.

Kuhusu ukarabati wa nyumba zao, Saguya amesema shirika hilo litaendelea kutekeleza mpango maalum wa miaka mitano wa ukarabati wa nyumba za shirika hilo unaoishia mwaka 2027.

Amesema watakarabati nyumba katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Tabora, Arusha, Kigoma, Morogoro, Lindi, Tanga, Mbeya, Mwanza, Singida na Kagera kwa gharama ya Sh8 bilioni.