Ni bajeti ya madeni uchaguzi, Afcon
Bajeti itakavyokuwa
Dk Mwigulu alisema katika bajeti ya mwaka 2024/25, Serikali inapendekeza kutumia Sh49.34 trilioni sawa na ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24 ya Sh44.38 trilioni.
Alisema misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo inakadiriwa kuwa Sh5.13 trilioni.
Pia, alisema Serikali inakadiria kukopa Sh6.61 trilioni kutoka soko la ndani na Sh4.02 trilioni ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Sh2.59 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Pia, alisema Serikali inakadiria kukopa Sh2.98 trilioni kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
Dk Mwigulu alisema bajeti hiyo itapatikana kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya Sh29.85 trilioni, mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na wizara, taasisi na idara zinazojitegemea ni Sh3.40 trilioni na mapato ya Serikali za mitaa yakiwa ni Sh1.34 trilioni.
Alisema kati ya bajeti ya Sh49.34 trilioni, Sh33.55 trilioni zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh15.78 trilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, sawa na ongezeko la asilimia 3.8.
Alisema fedha za maendeleo zinajumuisha ruzuku ya maendeleo ya Sh1.23 trilioni kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya kati na ya juu pamoja na programu ya elimu msingi na sekondari bila ada.
“Sehemu kubwa ya bajeti asilimia 70.1 itagharamiwa na mapato ya ndani ambayo yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 10.0 mwaka 2024/25. Hivyo, Serikali itaendelea kuweka msukumo na jitihada za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani,” alisema Dk Mwigulu.
Pia, alisema Serikali itaendelea kuhakikisha fedha za mikopo zinaelekezwa kwenye miradi ya kimkakati yenye matokeo ya haraka (quick wins) na manufaa mapana kwa Taifa (multiplier effect) ikiwamo kuongeza fursa za ajira, wigo wa mapato ya Serikali na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
Mpango kuzingatia misingi 10
Akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Taifa wa mwaka 2024/25, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema mpango huo utazingatia misingi 10.
Aliitaja misingi hiyo kuwa ni kuendelea kuwepo kwa amani, usalama na utulivu wa ndani ya nchi, nchi jirani na duniani kwa jumla pamoja na kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya fedha na bidhaa.
Misingi mingine ni kuendelea kudumisha utawala bora na wa sheria nchini, kuendelea kuimarika kwa utoshelevu wa chakula na kuendelea kuongeza kwa ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za uwekezaji na biashara.
Profesa Kitila alisema msingi mwingine ni kuendelea kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili na yasiyo ya asili kama ukame, vita, magonjwa ya mlipuko na mafuriko.
“Pia, kuwa na rasilimali watu wa kutosha na bora inayokidhi matakwa ya wakati ambayo yanatawaliwa na teknolojia na ubunifu na nidhamu katika matumizi ya fedha za umma,” alisema Profesa Kitila.
Alitaja misingi mingine ni kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, hususani kwa wafanyabiashara na wawekezaji wadogo na wakati wa ndani na kuwa na nidhamu ya utekelezaji wa mambo waliyopanga.
Profesa Kitila alisema Serikali imeweka kipaumbele katika kukamilisha miradi ya kielelezo pamoja na programu na miradi ya maendeleo inayoendelea, hasa iliyo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Alisema lengo ni kuwianisha uhalisia wa mapato na matumizi ya Serikali ili kufikia matokeo tarajiwa ya utekelezaji wa miradi katika kipindi cha ukamilishaji wa Dira ya 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).
Profesa Kitila alisema katika kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana katika utekelezaji wa miradi, Serikali imeimarisha mfumo wa tathimini na ufuatiliaji na sasa katika kila wizara ya kisekta na taasisi za Serikali zinazojitegemea, kuna idara inayohusika na tathmini na ufuatiliaji (M & E).
Profesa Kitila alisema, pia wataendelea kuhamasisha watekelezaji wa miradi kutumia Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo (NPMIS) ili kuhakikisha taarifa za miradi na programu zinapatikana kwa wakati hasa wakati wa ufuatiliaji na tathimini.
Awali, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alisema ili kamati ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, Serikali inapaswa kuwasilisha nyaraka zote kwa wakati na mawaziri wahudhurie vikao vya kamati za Bunge kwa kadri ratiba zilizopangwa.
“Ni matumaini yangu kuwa kamati zitazingatia ratiba zake na wajumbe wote watazingatia muda na kuhakikisha kazi zote za uchambuzi zilizopangwa zinakamilika kwa wakati ili kuwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake,” alisema Zungu.
Akitoa maoni yake kuhusu vipaumbele vya bajeti ijayo, Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi, Oscar Mkude alisema vipaumbele vilivyotolewa na Serikali si vibaya lakini ni vya kawaida.
“Hakuna kipaumbele unaweza kusema ni kielelezo mfano kama ilivyo miaka ya nyuma tulivyoona ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ni mradi wa kipaumbele kwa sababu inakwenda kushusha gharama za biashara na usafiri,” alisema Mkude.
Alisema jambo la muhimu la kuzingatiwa zaidi ni uchaguzi kufanyika kwa huru na haki ili kuepusha kuurudia kutokana na gharama zake kuwa kubwa.
Jambo lingine, alisema Serikali inapaswa kuwekeza kwenye udhibiti wa matumizi, akitolea mfano ununuzi wa magari mapya kila mara yanapoingia sokoni.
“Kwenye ukarabati wa magari Serikali inatumia magari mengi sana, hii ni gharama tofauti na magari mapya yanayonunuliwa ambayo yakitumika ndani ya muda mfupi, yanauzwa kwa bei ndogo sana na upo mchezo unafanyika wa kuuziana, hivyo natamani hili eneo lipewe kipaumbele kupunguza matumizi,”alisema Mkude.
Mwaka 2022/23 wakati akiwasilisha bungeni bajeti kuu ya Taifa, Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali hutumia Sh558 .4 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari, ukarabati vipuri na matengenezo kwa mwaka.
Dk Mwigulu alisema kwa mwaka huo wa fedha, Serikali ilikuwa na magari 15,742, pikipiki 14,042 na mashine 373.
Profesa wa Uchumi na Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Abel Kinyondo alisema wakati wa uchaguzi ni ngumu kufanyika jambo lingine litakaloonekana kubwa.
“Ndio maana tunashauri kama wanavyofanya wenzetu, kwa nini uchaguzi tusifanyike mara moja, mfumo uliopo sasa, mwaka huu tunafanya uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwaka unaofuata tunafanya Uchaguzi Mkuu, kazi ni zilezile, sasa kwa nini tusiwe na mwaka mmoja ambao watu watafanya uchaguzi,”alisema.
Profesa Kinyondo alisema ndani ya mwaka mmoja inawezekana kufanya uchaguzi wote kwa kuwa kuendelea na mfumo uliopo sasa ni kufanya malipo mara mbili kwa jambo moja.
“Uchaguzi unapofanyika kuna muda wa kampeni, ni kama kusimamisha shughuli za watu, sasa katika kupunguza matumizi ni vyema tukutanishe hizi chaguzi tuwe na uchaguzi mmoja kwa wakati mmoja, itasaidia sana kupunguza matumizi na kuruhusu vitu vya maendeleo kufanyika badala ya kuwa na miaka miwili ya kampeni na matumizi makubwa ya fedha,” alisema.
Nyongeza na Baraka Loshilaa