Njombe wajipanga kupunguza vifo vya wanawake na watoto

Friday May 13 2022
njombeepiic
By Seif Jumanne

Njombe. Mkoa wa Njombe unatarajia kupunguza vifo vya akina mama na watoto kwa kiwango kikubwa baada ya kupata daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na watoto.

Hayo yamesemwa na mganga mkuu wa mkoa wa Njombe Dk Zabron Masatu wakati wa uzinduzi wa kituo cha afya cha Marie stopes kilichopo mjini Makambako mkoani Njombe.

Amesema pamoja na kuwa mkoa wa Njombe kuwa na vituo 316 ambavyo kati yake vituo 296 vinatoa huduma za afya ya mama na mtoto lakini bado kuna changamoto zinazozuia utolewaji wa huduma kufikia viwango vinavyokidhi ikiwemo uhaba wa madaktari bingwa.

Amesema kupitia kituo hicho cha afya sasa huduma za kibingwa zitakuwa zikitolewa kwakuwa kuna daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na watoto.

"Hili ni jambo la kujivunia kwasababu tunahitaji kuwa na madaktari bingwa na vifaa vya kisasa ambavyo tutavitumia ili kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma bora," amesema Dk Masatu.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Njombe, Waziri Kindamba amesema serikali inafanya jitihada nyingi katika kuhakikisha inaboresha huduma za afya kwa wananchi kwa kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini.

Advertisement

"Hii ndiyo maana halisi ya ushirikiano baina ya sekta binafsi pamoja na serikali katika mambo yanayogusa maisha ya wananchi,” amesema Kindamba.

Naye Mkuu wa maendeleo kutoka ubalozi wa Canada ambao ndiyo wafadhili wa kituo cha afya Marie stopes, Helen Fytche amesema ujenzi wa kituo hicho ni mwendelezo wa jitihada za shirika hilo kusogeza huduma hasa za afya ya uzazi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Amesema Canada ni mdau wa muda mrefu hapa nchini na wameshatoa zaidi ya dola 510 kwenye sekta ya afya kwa miaka kumi iliyopita.

"Canada ilianza rasmi kufuata sera ya kimataifa ya kijinsia mwaka 2017 ili kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia kiini katika kusaidia maendeleo" amesema Helen.


Advertisement