North Mara yakamuliwa Sh40 bilioni

Muktasari:

Mahakama Kuu (Divisheni ya Biashara) imeiamuru kampuni ya uchimbaji madini ya North Mara Gold Mine Limited (NMGM) kuwalipa wachimbaji wazawa Dola za Marekani 17.4 milioni (Sh40 bilioni) ikiwa ni malimbikizo ya mrahaba wa dhahabu waliyochimba na kuuza kutoka kwenye eneo walilokabidhiwa na wananchi hao kwa makubaliano maalumu.


Dar es Salaam. Mahakama Kuu (Divisheni ya Biashara) imeiamuru kampuni ya uchimbaji madini ya North Mara Gold Mine Limited (NMGM) kuwalipa wachimbaji wazawa Dola za Marekani 17.4 milioni (Sh40 bilioni) ikiwa ni malimbikizo ya mrahaba wa dhahabu waliyochimba na kuuza kutoka kwenye eneo walilokabidhiwa na wananchi hao kwa makubaliano maalumu.

Jaji Deo Nangela amekubaliana na hoja za kampuni ya Isaac & Sons kwamba kwa miaka 23, NMGM imekuwa ikikiuka masharti ya mkataba uliowataka wailipe kampuni hiyo mrahaba wa asilimia moja kwa dhahabu wanayouza.

Mahakama hiyo imesema pia makubaliano yaliyoipa NMGM haki zote (exclusive rights) za uchimbaji madini kwenye eneo ambalo awali lilimilikwa na wazawa hao umegubikwa na usiri na utata.

Tayari, NMGM imetoa taarifa ya kukata rufaa kupinga uamuzi huo ambao umevuta hisia za wadau wengi katika sekta ya madini.

“Kwa kuwa ni dhahiri mdaiwa (NMGM) amechimba na kujenga tuta kubwa katika eneo linalochimbwa madini ambalo awali lilimilikiwa na kuwanufaisha walalamikaji (Isaac & Sons), hakuna shaka kuwa walalamikaji wanastahili malipo ya mrahaba,” alisema Jaji Nangela katika hukumu ya kurasa 91.

Isaack & Sons inayomilikiwa na kuendeshwa na Watanzania watano, wakiwamo Josephati Isaac Mwita, Enock Isaac Mwita na wengine watatu, ilifikia uamuzi wa kuishtaki NMGM Desemba 2020 baada ya kuituhumu kwa kushindwa kuwalipa asilimia moja ya mrahaba, waliyodai ilikuwa imefikia Dola za Marekani 21.6 milioni hadi kufikia Juni 30, 2017.


Hoja za Isaack & Sons

Nyaraka za kesi na rekodi za Mahakama zinaonyesha kuwa kampuni ya Isaac & Sons ndiyo iliyokuwa mmiliki na mnufaika wa haki zote za chini na juu ya ardhi katika eneo ambalo sasa linaendeshwa kwa Leseni Kubwa ya Uchimbaji Madini (Special Mining Licence) wilayani Tarime, chini ya kampuni ya NMGM.

Kwa miaka mingi, eneo hilo lilikuwa likiendeshwa na wachimbaji hao wadogo hadi Septemba mwaka 1999 walipokubaliana kuhamisha haki za uchimbaji madini kwa NMGM, kupitia mikataba mitatu tofauti.

Makubaliano hayo yaliipa NMGM haki zote (exclusive rights) za kufanya shughuli za uchimbaji madini katika maeneo hayo.

Katika moja ya kipengele muhimu cha makubaliano hayo, NMGM ilikubali kuilipa kampuni ya Isaack & Sons mrahaba wa asilimia moja ya dhahabu yote watakayochimba katika maeneo ya mkataba na kuuza.

“Ingawa mdaiwa amezalisha kiasi kikubwa cha dhahabu tangu alipoanza shughuli za uchimbaji, mlalamikaji hajawahi kupewa taarifa zozote kuhusu uzalishaji wa dhahabu katika eneo la mkataba,” alidai mmoja wa wakurugenzi na mwanahisa wa Isaac & Sons, Enock Isaac Mwita (74).

Kampuni hiyo ilidai kuwa hadi kufikia Juni 30, 2017 walikuwa wanastahili kulipwa malimbikizo ya mrahaba kiasi cha Dola za Marekani 21.6 milioni.

Isaac & Sons walidai pia walistahili kulipwa malimbikizo ya mrahaba kwa mwaka 2018, 2019 na 2020 na miaka iliyofuata hadi siku mgodi huo utakapofungwa rasmi.



Utetezi wa NMGM

NMGM haipingi ukweli kuwa waliingia mikataba mitatu na wachimbaji hao ambao walikubali kusalimisha na kuachia haki zao katika maeneo hayo, lakini wanasisitiza hawajawahi kuzalisha dhahabu kutoka kwenye maeneo hayo tangu mwaka 2013.

Shahidi mmoja wa NMGM, Alex Kaizirwa aliiambia Mahakama kwamba kampuni yao imekuwa ikizalisha dhahabu kutoka maeneo mengine tofauti tofauti yanayomilikiwa na watu wengine na si walalamikaji.

Akilifafanua hilo, Mchambuzi wa masuala ya fedha wa NMGM, Joseph Rafael alitoa ushahidi kwamba kampuni yao haiwajibiki kuwalipa walalamikaji kwa sababu “hadi leo hawajawahi kuzalisha dhahabu kutoka katika yaliyokuwa maeneo yao.”

Kwa mujibu wa Rafael, NMGM kamwe haijawahi kupokea ombi lolote kutoka kwa mlalamikaji la kutaka apewe taarifa zinazohusu hali ya uzalishaji dhahabu kutoka kwenye maeneo yao ya awali.


Mahakama yaamua

Jaji Nangela alianza uchambuzi wa ushahidi na vielelezo kwa kuibua kasoro kwenye kile kilichoitwa tafsiri ya Kiswahili ya mikataba mitatu, ambayo iliandaliwa na NMGM bila uwepo wa mlalamikaji na vipengele vya usiri katika mikataba hiyo.

Awali, Mahakama iliambiwa kuwa tafsiri ya Kiswahili ya mikataba hiyo ilisomwa kwa walalamikaji na mmoja wa maofisa usalama wa NMGM, Abiha Emmanuel, akieleza kuwa tafsiri hiyo ilikuwa ya kweli na sahihi ya mikataba ile mitatu.

“Hapakuwa na uthibitisho kwamba ofisa huyo wa usalama wa walalamikiwa alikuwa na weledi katika lugha za Kiswahili na Kiingereza kiasi cha kuifanya Mahakama hii iamini kuwa walalamikaji walielewa kilichokuwa kinatafsiriwa. Walalamikiwa hawakujishughulisha hata kumleta mtu huyo mahakamani kutoa ushahidi kwenye hilo,” alisema jaji.


Maneno mazito

Alisema ushahidi uliotolewa mahakamani ulionyesha wazi kuwa kwa kiasi kikubwa mzania wa meza ya kujadiliana katika mikataba hiyo uliegemea katika kupendelea upande ulioandaa mkataba.

“Nakubaliana na hoja za mawakili wa wadai kuwa katika mazingira kama hayo, ukiongeza na viashiria vyote vya uwepo wa nguvu ya majadiliano isiyo sawa, vinavyodaiwa kuwa vigezo vya makubaliano hayo lazima visomwe kwa tahadhari kubwa. Utata wowote lazima uamuliwe kwa faida ya mlalamikaji ambaye si aliyeandaa mkataba huo.

“Hakika, hilo ni lazima kwa sababu biashara nyingi za uchimbaji madini katika sehemu mbalimbali nchini zimegubikwa na hatari ya kutokuwepo usawa katika majadiliano na kugubikwa na ujanja, ambapo kosa moja linaweza kusababisha kukaliwa kwa ardhi yenye madini ya thamani bila ruhusa.

“Zaidi ya hayo, baada ya kuandaliwa, mikataba hiyo imelindwa na vipengele vya usiri kama kipengele cha tano cha mikataba hiyo mitatu. Usiri huo umekuwa na umeendelea kuwa chanzo cha uvunjifu wa haki katika sekta ya uchimbaji madini na inalazimisha zama mpya ya uwazi katika sekta hiyo,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji, namna kipengele cha tatu cha mkataba kati ya Isaac & Sons na NMGM kilivyoandaliwa imechochea kwa kiasi kikubwa tabia ya usiri na ufichaji wa taarifa, hivyo kumwacha mlalamikaji katika giza na sintofahamu kifedha.

Jaji Nangela pia alikataa utetezi wa NMGM kuwa hawakuilipa kampuni hiyo ya wazawa kwa kuwa walikuwa bado hawajaanza shughuli za uchimbaji katika eneo husika. “Ni maoni yangu thabiti kuwa si tu kwamba mdaiwa alikwishaanza shughuli za uchimbaji madini katika eneo la mkataba, lakini pia mdaiwa anazalisha dhahabu kupitia shughli hizo,” alisema.

Mahakama hiyo pia imeiamuru NMGM kuwalipa wadai Sh300 milioni ikiwa ni hasara ya jumla (general damages) iliyotokana na kukiukwa kwa mkataba.

NMGM wameamriwa kulipa riba ya asilimia saba ya Dola za Marekani 17.4 milioni kuanzia siku hukumu hiyo iliposomwa hadi tarehe ya malipo ya mwisho ya fedha wanazodaiwa.