Nusu kidato cha nne wapata daraja la IV

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ilboru ya mkoani Arusha wakishangilia baada ya kupata taarifa shule yao imeshika nafasi ya pili katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne 2020.

Dar es Salaam. Wakati matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa Januari 15 mwaka huu yakionyesha ufaulu kupanda kwa asilimia 5.19, nusu ya waliofanya mtihani huo wamepata daraja la nne.

Kufuatia wingi wa waliopata daraja hilo, wadau wa elimu wamezungumzia sababu na kutoa mapendekezo ya hatima yao.

Kulingana na takwimu na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) watahiniwa 221,049 sawa na asilimia 50.74 wamepata daraja la nne, kati yao wasichana ni 126,773 na wavulana 94,276.

Idadi hiyo ni ongezeko la asimia 2.68 ya watahiniwa waliopata daraja hilo katika mtihani uliofanyika mwaka 2019 ambapo wanafunzi 205, 613 sawa na asilimia 48.6 walipata daraja la nne.

Wakati takwimu zikiwa hivyo kwa daraja la nne, jumla ya watahiniwa 61,696 walipata daraja sifuri ikiwa ni pungufu kwa asilimia tano ya waliopata daraja hilo mwaka 2019, ambapo wahitimu 81,808 walipata sifuri.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi jana, wadau wa elimu wamesema idadi hiyo inaonyesha kuna kundi kubwa la vijana watakaoshindwa kusonga mbele kwenye ngazi mbalimbali za elimu kwa kuwa daraja la nne halimuwezeshi mtu kuchaguliwa katika shule ya Serikali.

Akizungumzia suala hilo la wingi wa watahiniwa waliopata daraja nne, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Faraja Kristomus alieleza kuwa hali hiyo inaleta taswira kuwa kuna changamoto kwenye mfumo wa ufundishajI.

Alisema mfumo wa kufundishia ukibadilishwa kutoka kwenye kukariri hadi umahiri bado walimu wengi waliopo pembezoni mwa nchi wanakuwa hawajapata mafunzo ya kutosha kuhusu mfumo huo hali inayowasababishia kuendelea kufundisha kizamani.

“Katika shule nyingi za pembezoni walimu hawana mafunzo ya mfumo huu wa kumjenga mwanafunzi kwenye umahiri, shule pia hazina mazingira wezeshi yanayomfanya mtoto atumie umahiri wake katika kujifunza na kwa bahati mbaya mitihani ikija inakuwa imetungwa kwa mfumo huo,” alisema Faraja.

Kwa upande wake, kiongozi mstaafu wa Chama cha Walimu (CWT), Ezekiah Oluoch alisema hali hiyo inachangiwa na ongezeko la wanafunzi shuleni ambayo haiendani na ongezeko la walimu.

Oluoch alisema shule nyingi zipo katika mazingira magumu ya kufundishia na kujifunza hali inayochangia namba ya wanafunzi wanaopata daraja la nne na sifuri kuendelea kuwa kubwa.

“Shule zaidi ya 4,000 zipo vijijini na kwenye ngazi ya kata ambako mazingira ya kufundishia ni magumu, walimu wachache na hawapati motisha, vitabu havipatikani kulingana na uwiano wa wanafunzi, hata watoto kukaa muda mrefu bila kupata chakula inawapotezea morali ya kuzingatia kinachofundishwa.

“Katika hili, Serikali ikubali wazazi wachangie chakula shuleni ili watoto hata wakimaliza vipindi ile saa nane wabaki kujisomea hadi jioni. Hii itawasaidia hata wale ambao wakirudi nyumbani hawapati nafasi ya kusoma kutokana na mazingira,” alisema Oluoch.


Kundi hili linasaidiwaje

Kwa kuwa si wote watakaopata fursa ya kuendelea na kidato cha tano kwenye shule za binafsi, wadau wameshauri vyuo vya ufundi kuongezewa uwezo ili viweze kuwachukua kwa wingi.

“Hapa ndipo vyuo vya ufundi vinapoingia. Hawa wanatakiwa kwenda kwenye kozi za kujiajiri ili wakitoka huko waweze kujiajiri na si kurudi mtaani tena kusubiri ajira.

“Ni muhimu vyuo vya ufundi na kati viwe vingi, maana ili nchi yetu iweze kuendelea tunahitaji asilimia 65 ya Watanzania wawe na ujuzi katika fani mbalimbali, ‘‘ alisema.