Nyalandu: Magenge ya mitandaoni yamefupisha safari yangu Chadema

Nyalandu: Magenge ya mitandaoni yamefupisha safari yangu Chadema

Muktasari:

  • “Magenge ya mitandao ya jamii” yamekatisha safari ya Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kurejea CCM.

Dodoma. “Magenge ya mitandao ya jamii” yamekatisha safari ya Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kurejea CCM.

Nyalandu alitangaza uamuzi wa kurejea CCM Aprili 30, mwaka huu jijini Dodoma wakati wa mkutano mkuu maalumu uliomchagua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Kama alivyorudi CCM, mwanasiasa huyo ambaye alijitosha mara mara mbili katika vyama tofauti kuomba kuteuliwa kuwania urais – CCM 2015 na Chadema 2020, ndivyo Oktoba 30, 2017, alivyojiondoa CCM na kujiunga na Chadema.

Hata hivyo, taarifa ya mbunge huyo wa zamani wa Singida Kaskazini ya kutangaza kukujiondoa CCM, ilikuwa tofauti na ile iliyotolewa bungeni na Spika Job Ndugai ambaye alisema ofisi yake ilipokea barua kutoka kwa Katibu mkuu wa CCM ikimtaarifu kwamba Nyalandu amepoteza sifa ya kuwa mwanachama wa chama hicho kwa utovu wa nidhamu.

Miongoni mwa mambo yaliyoelezwa wakati huo ni kwenda Nairobi nchini Kenya kumjulia hali aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye alikuwa amelazwa huko akitibiwa majeraha ya risasi alizopigwa akiwa Dodoma. Juzi jijini hapa Nyalandu alifanya mahojiano maalumu na gazeti hili akisema uamuzi wa kujiondoa Chadema hakuufikia kwa siku moja bali tangu Machi mwaka huu baada ya tafakari ya kina.

Nyalandu hadi anajiondoa Chadema alikuwa mwenyekiti wa Kanda ya Kati na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho. “Nikiwa nchi ya ugenini (Chadema) nikaanza kuona kulikuwa na tunu fulani ambazo ninazikosa nilizokuwa nazifahamu. Kwa mfano kama ukitofautiana jambo na mwenzako mwenye itikadi tofauti husimami na kuanza kumtukana au kumpasha maneno ya kumkwaza au kumkejeli,” alisema Nyalandu, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Nyalandu alisema hatua ya kuwa kwenye chama cha siasa ambacho kila mtu anaweza kumvunjia mwenzie heshima kwake yeye kulimfanya ‘wimbo kutoimbika ugenini’. Alisema kwake yeye hata mtu akimkwaza atatafuta namna nzuri ya kumwambia, lakini hatomtupia maneno yasiyostahili. “Na ndio maana kuja kwangu CCM, mtu yoyote wa Chadema hata aniudhi namna gani, hata uende mtandaoni umtukane Nyalandu.

Povu likutoke unapoteza muda wako tu, kwa sababu mimi sitakujibu maneno ya kejeli, sitakukwaza,” aliongeza Nyalandu, ambaye ambaye juhudi za kuwania ubunge na urais kupitia Chadema hazikufua dafu.

 Alisema Watanzania wengi walio katika vyama vya siasa ni wazuri na kwamba wana matarajio, matamanio na jambo lao ambalo linaweza kuwa ni masuala ya afya, elimu au maji. Hata hivyo, alisema masuala hayo yanaweza kuwekwa katika sera za vyama katika majibishano yenye hekima na misingi.

 “Sasa upande wa pili (Chadema) tulitofautiana sana na namna tunavyoweza tukajadili mambo fulani fulani,” alisema Nyalandu. Sababu za kurudi CCM Alisema alitazama misingi iliyopo CCM na changamoto ambazo walikuwa wakizipata upinzani akaona kuna haja ya chama cha siasa kutotengeneza alichoita magenge ya wababe mitandaoni.

 “Magenge ya wababe katika siasa ni kwamba kila kiongozi akipanda tu anakuwa na genge lake, genge hili liko mitandaoni hajapenda kitu, analituma kukutukana na mwenye genge la pili naye anatumwa kumtu[1]kana mwenzake,” alisema.

 Alisema ndio maana kila wakati kunakuwa na vurugu za mitandaoni zinazotokana na aina fulani ya watu kutengeneza magenge yao ili waweze kuendelea kuwa viongozi ama kuendelea kuwa na ushawishi wa kutumia watu wengine. Hata hivyo, alisema yeye haamini kuwa utaratibu huo wa kutumia magenge unaweza kuleta ushindi endelevu.

Nyalandu alitoa mfano wakati ambapo Taifa lilikuwa likijaribu kujua Hayati John Magufuli anaumwa nini, magenge ya mtandaoni yalianza kusherekea. “Huyu ni kiongozi mkuu wa nchi, ndio Amiri Jeshi Mkuu ndio baba yetu, magenge ya mtandaoni yalianza kusherekea na wapo hadi sasa walikuwa wanashangilia. Wengine wanasema kama yeye alikuwa anasali tumwone sasa. Watu wengine wananunua pombe wanalewa hadi asubuhi.

“Lakini, mimi niwasaidie watu, mwenye mamlaka ya juu ya kuleta uhai wa mwanadamu na kuondoa saa anayotaka wa kwako na mwenzako ni Mungu pekee. Wote tumeletwa duniani kwa kusudi la Mungu hata kama umpende au umchukie,” alisema.

 Alipoondoka CCM Septemba, 2017, Nyalandu alipotangaza kujiondoa CCM alitoa taarifa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook akisema alichukua uamuzi huo kutokana na kutokuridhishwa na mwenendo wa siasa nchini Tanzania Alisema kumekuwa na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya kidhalimu dhidi ya raia na kutokuwepo kwa mipaka baina ya mihimili ya dola - Serikali, Bunge na Mahakama.

“Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya sasa, hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali,” aliongeza.