Nyati mweupe aonekana Tarangire, avutia mamia ya watalii

Nyati mweupe akiwa ndani ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire

Muktasari:

Nyati mweupe ameonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kuwa kivutio kwa watalii wa ndani na nje ya nchi wakitaka kumuona.

Tarangire. Nyati mweupe ameonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kuwa kivutio kwa watalii wa ndani na nje ya nchi wakitaka kumuona.

Nyati huyo ambaye kwa mara ya kwanza ameonekana jana Jumatatu Mei 16, 2022 jioni ndani ya hifadhi hiyo amesababisha watalii wengi waliokuwa hifadhini kuanza kumfatilia na kuanza kuvutia watafiti katika eneo hilo.

Mmoja wa mashuhuda wa nyati huyo, Jeremiah Peter amesema nyati huyo ni mkubwa tofauti na nyati wengine katika hifadhi hiyo na ameonekana akikaa katikati ya nyati wengine.

"Haya ni maajabu mengine katika utalii wa Tanzania tunaimani huyu nyati atavutia watalii" amesema

Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete amesema nyati huyo ameonekana kwa mara ya kwanza jana na amekuwa kivutio kwa wengi.

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha huenda nyati huyo ni albino sawa na wanyama wengine weupe waliowahi kuonekana katika hifadhi hiyo akiwemo twiga.

"Tutaendelea kumfatilia na kumtunza nyati huyo kwani tangu habari zake zimejulikana kuna wengi wameanza kufatilia" amesema Shelutete.

Mbunge wa zamani wa Jimbo la Babati, Jitu Song amesema nyati huyo ni kuvutio kizuri cha utalii kwa sasa Tarangire.

"Ameonekana jana na watu waliokuwa hifadhini na amekuwa kivutio kikubwa sana ingawa tayari waliwahi kuonekana wanyama weupe katika hifadhi hiyo tofauti na rangi yao ya asili" amesema.