Nyuki wazua taharuki uchaguzi CCM Mbeya

Muktasari:

Tukio hilo lilitokea jana Oktoba 2, 2022 wakati wa mapumziko na wajumbe wakisubiri utaratibu wa kurudia kwenye uchaguzi baada ya wagombea kutofisha idadi ya kura zinazotakiwa.

Mbeya. Katika hali isiyo ya kawaida, nyuki wamevamia ukumbi wakati uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbeya Vijijini.

Tukio hilo lililotokea jana Oktoba 2, 2022 liliwashangaza wengi wakati wa mapumziko na wajumbe wakisubiri utaratibu wa kurudia uchaguzi baada ya wagombea kutofikia idadi ya kura stahiki.

Kabla ya kurudiwa kwa uchaguzi huo, wagombea walikuwa watatu akiwemo Akimu Mwalupindi, Japhet Mwanasenga na Ramadhan Mwandala ambapo mshindi alipaswa kufikisha nusu ya kura za wajumbe.

Katika kura za awali kabla ya uchaguzi kurudiwa, Mwalupindi alipata kura 682, Mwanasenga kura 500 na Mwandala alipata kura 218, jambo ambalo lilimfanya msimamizi kuamuru uchaguzi urudiwe.

Wakati uchaguzi ukirudiwa, hali ilibadilika ukumbini baada na nyuki ambao haikufahamika walipotoka kuzingira ukumbi huo na kuwafanya wajumbe kutawanyika na kukimbia bila kupiga kura.

Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya, Jacob Mwakasole alithibitisha kutokea tukio hilo na kwamba tukio hilo liliwaacha na mshangao kwani wajumbe wawili waliumia na kupelekwa hospitali.

“Nyuki hao walitokea tukitoka kupata chakula kuelekea kwenye marudio ya uchaguzi, tulishangaa kuona kila mtu kwenye makoti yake na ukumbi mzima kuwa na wadudu hao hadi kuleta taharuki na wajumbe kukimbia,” alisema Mwakasole.

Naye Mwalupindi aliyeshinda nafasi ya mwenyekiti, alikiri kutokea tukio hilo huku akieleza kuwa baada ya kutokea tukio hilo kila mmoja alianza kuwaza anavyojua mwenyewe kwa kuwa siyo tukio la kawaida.

“Kwanza nashukuru wajumbe kwa kunipa ridhaa, tushirikiane kuchapa kazi, mimi hizo nyuki sikujua zilitoka wapi hadi nikahisi wapiga kura wangu wataondoka,” alisema Mwalupindi.