Nyuma ya pazia kolabo Diamond Platnumz na Koffi Olomide

Nyuma ya pazia kolabo Diamond Platnumz na Koffi Olomide

Muktasari:

Novemba 25 mwaka huu msanii wa Bongo fleva, Diamond Platnumz aliachia wimbo wake mpya aliomshirikisha mkongwe wa muziki Afrika, kutokea DR Congo, Koffi Olomide, inayokwenda kwa jina la Waah!.

Novemba 25 mwaka huu msanii wa Bongo fleva, Diamond Platnumz aliachia wimbo wake mpya aliomshirikisha mkongwe wa muziki Afrika, kutokea DR Congo, Koffi Olomide, inayokwenda kwa jina la Waah!.

Kolabo hiyo na mkali huyu wa muziki wa Soukus inakuja siku chache mara baada ya Kofii kumtembelea Diamond nchini na mara moja wakaigia studio na kufanya jambo lao, lakini kwa nini Koffi Olomide?, karibu nikuonyeshe kilichopo nyuma ya pazia.

Ukweli ni kwamba nyimbo ambazo Diamond amefanya na wasanii wa DR Congo zimekuwa na mafanikio makubwa ukilinganisha na zile alizofanya na wasanii kutokea mataifa mengine kama Nigeria, Afrika Kusini, Kenya, Marekani n.k.

Kipimo ambacho kimekuwa kikitumiwa na wasanii wengi nchini kutoa ishara ya wimbo uliofanikiwa ni idadi ya waliotazama katika mtandao wa YouTube, ingawa njia hii imekuwa akikabiliana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wasanii waliofanya Bongofleva toka miaka ya 2000 na kufanikiwa vilivyo.

Rapa Roma Mkatoliki anaeleza kuwa wasanii wataendelea kutumia njia hiyo kutokana Bongofleva kukosa tuzo tangu kusitishwa kwa Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA), hakuna namna zaidi ya hapo!.

Naye Diamond ameamua kupima kolabo zake za kimataifa kwa kutumia njia hiyo. Kolabo alizofanya na nnoss’B na Fally Ipupa zimekuwa na mafanikio makubwa YouTube kuliko zile alizofanya na Davido, Mr. Flavour, Iyanya, Patoranking, P Square, Ne-Yo, Omario, Rick Ross n.k.

Video ya wimbo “Yope Remix” alioshirikishwa na Innoss’B uliotoka Septemba 7, 2019 imetizamwa zaidi ya mara milioni 125 tangu itoke ikiwa ndio video pekee katika chaneli ya Diamond kutazamwa zaidi ya mara 100 milioni. Hii ni rekodi kubwa na mafanikio hayo yamepatikana ndani ya mwaka mmoja.

Hiyo ilikuwa ni baada ya Diamond kufanya kolabo nyingine na Fally Ipupa kutokea huko huko Congo, hadi sasa video ya wimbo huo “Inama” iliyotoka Juni 9,2020 imetizamwa katika mtandao wa YouTube zaidi ya mara 76 milioni ikiwa ni video yake ya pili kutazamwa zaidi katika chaneli yake.

Kolabo hizi mbili alizofanya na wakali hawa kutokea DR Congo, ndani ya mwaka mmoja zimevunjilia mbali rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na “Nana’ kolabo aliyofanya na Mr. Flavour kutokea Nigeria miaka mitano iliyopita. Video ya wimbo “Nana” iliyotoka Mei 29, 2015 hadi sasa imetizamwa zaidi ya mara 68 milioni.

Kutokana na mafanikio hayo, toka mwaka jana Diamond amekuwa anajikita kufanya kolano na wasanii kutoka DR Congo ili kuendeleza moto wake huo aliyouwasha mwenyewe.

Lakini kwa nini wasanii wa DR Congo pekee ndio wanamleta mafanikio haya na sio mataifa mengine?.

Kwa mujibu wa mtandao wa kutoa takwimu za papo hapo, Worldometers inakadiri nchi ya DR Congo kuwa idadi ya watu zaidi ya milioni 89.5. Watu wao wanazungumza Kifaransa kama lugha rasmi, pia kuna Kikongo (Kituba), Kilingala, KiTshiluba na Kiswahili, huku kukiwa na lugha zaidi ya 200 za makabila mbalimbali.

Kiswahili kutumika nchini DR Congo kunamuongezea Diamond, uwanja wa kuuza muziki wake na ndio sababu ya kolabo anazofanya na wasanii kutokea nchini humo kufanya vizuri.

Hii ni faida kuliko anapofanya kazi wasanii kutokea nchini kama Nigeria na Marekani ambapo wanaofahamu Kiswahili ni wachache mno.

Sasa Diamond ikichukua idadi ya Watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 59, kwa mujibu wa Worldometers, na wale milioni 89 wa DR Congo ambapo idadi kubwa ya wanaotokea mataifa haya wanafahamu Kiswahili huoni hiyo ni kolabo biriani kabisa.

Mbinu hii ya pili, ndio aliyoitumia Beyonce kutokea Marekani kwa kuwajaza wasanii kama Tekno, Yemi Alade, Mr Eazi, Tiwa Savage, Wizkid na Burna Boy wote kutokea Nigeria katika albamu yake inayokwenda kwa jina la “Lion King”.

Mke huyo wa Rapa Jay Z alifahamu kuwa nchini hiyo ina idadi ya watu zaidi ya milioni 200 wanaofahamu lugha ya Kingereza hivyo atapata mafanikio makubwa zaidi kisoko.