Odinga ‘akacha’ utangazwaji matokeo urais Kenya

Mgombea wa urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga

Muktasari:

  • Wakala mkuu wa Azimio la Umoja, ambalo lilimsimamisha Raila Odinga kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022 amesema mgombea wao hawezi kwenda katika ukumbi wa Bomas ambapo mshindi wa kiti cha urais atatangazwa.

Nairobi. Wakala mkuu wa Azimio la Umoja, ambalo lilimsimamisha Raila Odinga kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022 amesema mgombea wao hawezi kwenda katika ukumbi wa Bomas ambapo mshindi wa kiti cha urais atatangazwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumatatu Agosti 15, 2022, wakala huyo, Saitabao Kanchory amesema hawayatambui matokeo ya uchaguzi yatakayotangazwa na IEBC mpaka uhakiki wa matokeo yote umalizike.

Kauli ya Kanchory imetolewa huku tayari viongozi mbalimbali, wanadiplomasia na maofisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya wakiwa ndani ya ukumbi wa Bomas kwa zaidi ya saa sita kusubiri kutangazwa matokeo hayo ambayo awali yalikuwa yatolewa saa 9 lakini hadi saa 10:20 yalikuwa bado hayajatangazwa.

“Kwa upande wetu matokeo ambayo bado hayajahakikiwa sio matokeo, Mwenyekiti wa IEBC aliahidi kuwepo kwa mchakato huru na wa haki kitu ambacho hakijafanyika,”amesema.

Madai ya mawakala wa Azimio la Umoja ni pamoja na kutokukamilika kwa mchakato wa uhakiki wa fomu zenye matokeo ya urais maarufu kama fomu namba 34A.

Aidha, ameongeza kuwa hawatamuita mgombea wao wa urais (Raila Odinga) mpaka uhakiki ukamilike wa matokeo hayo.

Kabla ya kujitokeza mbele ya vyombo vya habari nje ya ukumbi wa Bomas, Kanchory, Jumamosi Agosti 13, 2022 majira ya usiku alitolewa na polisi kwenye eneo la kuhesabia kura (auditorium) huku akilalamika kuwa ukumbi huo umekuwa eneo la uhalifu na kutoridhishwa na baadhi ya matukio yanayoendelea.