Odinga akataa matokeo ya urais Kenya

Aliyekuwa mgombea urais wa Kenya, kupitia wa Azimio la Umoja, Raila Odinga

Muktasari:

  • Aliyekuwa mgombea urais wa Kenya, kupitia wa Azimio la Umoja, Raila Odinga Raila, amekataa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022, yaliyotangazwa jana na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, Wafula Chebukati.

Nairobi. Aliyekuwa mgombea urais wa Kenya, kupitia wa Azimio la Umoja, Raila Odinga Raila, amekataa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022, yaliyotangazwa jana na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, Wafula Chebukati.
Jana, Chebukati alimtangaza mgombea urais kupitia Kenya Kwanza Dk William Ruto kuwa mshindi kwa kupata kura milioni 7.1 (asilimia 50.49) dhidi ya kura milioni 6.9 (asilimia 48.85) alizopata Odinga.
Wagombea wengine kwenye uchaguzi huo ni George Wajackoyah aliyepata kura 61,969 (asilimia 0. 44) na David Waihiga alipata kura 31,987
Hata hivyo leo, Odinga amezungumza na waandishi wa habari na kuweka wazi kuwa hatambui matokeo hayo na hamtambui Ruto kuwa ni Rais Mteule kwasababu amepatikana kutokana na matokeo batili.
Odinga amegombea urais wa Kenya mara tano ikiwamo uchaguzi uliofanyika Agosti 9, mwaka huu na mara zote alizogombea alishindwa na wapinzani wake.
Amesema kulikuwa na ukiukwaji mkubwa matokeo wakati wa uhesabuji kura lakini atatumia njia za kisheria kudai haki ya Wakenya iliyovurugwa na IEBC
Katika mkutano huo, Odinga amewataka wafuasi wake wawe watulivu na wasijichukulie sheria mkononi kwa kuwa nchi hiyo ina utaratibu mzuri wa kudai haki kupitia vyombo vya kisheria.

Amesema yeye na wenzake wa Azimio la Umoja walishtuka kuona Chebukati akiamua peke yake kumtangaza mshindi katika uchaguzi huo licha ya kwamba makamishna walio wengi walikataa kuhusika na matokeo hayo.

“Takwimu zilizotangazwa na Chebukati si halali na tutalishughulikia jambo hili katika mahakama ya sheria. Kitendo cha Chebukati kutangaza mshindi ni kinyume cha sheria na taratibu,” amesema Odinga.

Amebainisha kwamba sheria inayounda IEBC inaelekeza kwamba uamuzi katika jambo lolote utapitishwa na makamishna walio wengi. Hata hivyo, amesema jambo la kushangaza ni kwamba mwenyekiti huyo wa IEBC alitangaza matokeo licha ya makamishna wanne kujitenga.

Odinga amedai kwamba Chebukati pekee ndiyo alikuwa akipata matokeo ya uchaguzi. Aliwakatalia makamishna wengine kupata matokeo hayo hadi baadaye alipowapelekea rasimu ya mwisho aliyoitangaza.

Amesisitiza kwamba mwenyekiti huyo wa IEBC angeweza kusababisha machafuko kama siyo utulivu ulioonyeshwa na wafuasi wake. Amewataka wafuasi wa Azimio la Umoja kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati wanakwenda kushughulikia jambo hilo mahakamani.


“Wafuasi wetu waendelee kuwa watulivu. Tutafuata mkondo wa sheria kupinga matokeo yaliyotangazwa na Chebukati kinyume na katiba na sheria za Kenya,” amesema Odinga huku akishangiliwa na baadhi ya watu wake wa Azimio la Umoja.

Amesisitiza kwamba hawatakubali mtu mmoja ajaribu kuleta vurugu katika taifa ambalo sasa limetulia baada ya kupitia ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007/8 na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mwaka 2017.