Odinga amaliza ‘bata lake’ Zanzibar, awasha moto

Muktasari:

Siku chache baada kushindwa kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Kenya, Raila Odinga, aliyepata ridhaa hiyo kupitia Azimio la Umoja aliamua kwenda visiwani Zanzibar kujipumzisha na sasa amerejea nchini humo kuendelea na shughuli za kisiasa.

Mombasa. Siku chache baada kushindwa kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Kenya, Raila Odinga, aliyepata ridhaa hiyo kupitia Azimio la Umoja aliamua kwenda visiwani Zanzibar kujipumzisha na sasa amerejea nchini humo kuendelea na shughuli za kisiasa.

Raila hakuwapo kwenye sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Kenya William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua, zilizofanyika Septemba 13, 2022 katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.

Juzi Odinga alirejea nchini humo na akiwa uwanja wa ndege wa Mombasa alikutana na Naibu Rais, Gachagua kwa mara ya kwanza na kufanya mazungumzo.

Wawili hao walikutana juzi asubuhi kwenye uwanja wa kimataifa wa ndege wa Mombasa ambapo Odinga alikuwa akitokea Zanzibar huku Gachagua alikwenda kufungua mkutano wa baraza la magavana na Odinga alikuwa hapo kuhudhuria kuapishwa kwa gavana Abdulswamad Nassir.

Hata hivyo, taarifa za mazungumzo hayo hazikuwekwa bayana ingawa Gachagua, kwenye ukurasa wake wa Facebook aliandika; “Nimefurahi asubuhi hii kufanya mazungumzo na mzee wetu Waziri Mkuu mstaafu mheshimiwa Raila Amolo Odinga mjini Mombasa.

Pia, kwenye ukurasa wake Twitter, Gachagua ameandika: “Tuna heshima kubwa kwa wazee wetu. Nimefurahia leo kufanya mazungumzo na mmoja wa wazee wetu, Waziri Mkuu mstaafu mheshimiwa Raila Amolo Odinga mjini Mombasa.”

Odinga alikuwa mgombea urais kupitia Azimio la Umoja katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, akishindana na mpinzani wake wa karibu wa chama cha United Democratic Alliance (Uda), Dk William Ruto ambaye ndiye Rais wa tano wa Kenya na Gachagua ni Naibu Rais.

Hata hivyo, Odinga alipinga ushindi wa Ruto, Mahakama ya juu chini ya majaji saba wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome. Kesi hiyo ilitupwa baada ya majaji wote saba kwa kauli moja kukataa pingamizi lililowekwa na Odinga.


Awasha moto

Akiwa Mombasa juzi baada ya kurejea nchini akitokea Zanzibar kwa mapumziko na familia yake, Odinga alijibu taarifa kwa umma iliyotolewa na Mahakama ya Juu ikionya wale wanaoishambulia kwenye mitandao ya kijamii kwa uamuzi wake wa kutupa kesi ya Odinga. Odinga huku akionekana mwenye hasira, aliashiria huenda msimu wa maandamano ukarudi hivi karibuni.

“Tunaweza kuanzisha maandamano ya wananchi milioni moja hadi idara ya Mahakama na kuwaambia kwendeni nyumbani,” alisema Odinga kwenye sherehe za kuapishwa kwa gavana wa Mombasa.

Aliwataka Wakenya kuendelea kuilalamikia idara ya mahakama akisema hawezi kuruhusu iwahujumu Wakenya.

Kiongozi wa Azimio la Umoja ametishia kuanzisha maandamano ya kuwatimua majaji wa Mahakama ya Juu. Huku akidai idara ya mahakama inataka kugeuka na kuwa dikteta.

Odinga aliikosoa pia IEBC akisema ilitekeleza uchaguzi wa kughushi. “IEBC ni nyingine ambayo imeharibika na inafaa kufanyiwa mageuzi kamili,” alisema.

Alisema huenda Wakenya wakakosa kushiriki uchaguzi wa 2027 akidai kuwa mamluki walihusika kuamua Rais atakuwa nani.

Alisema wapiga kura wanatumia muda wao kwenye foleni lakini baadaye uchaguzi unakorogwa.