Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ofisa TRC aliyepinga tozo za miamala ya simu afukuzwa kazi

Jonas Afumwisye

Muktasari:

  • Wakati kilio cha tozo za miamala kikiendelea mtaani, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limemfukuza kazi meneja wake wa kanda ya Dar es Salaam, Jonas Afumwisye kwa kuzipinga kwenye makundi ya kijamii.

Dar es Salaam. Wakati kilio cha tozo za miamala kikiendelea mtaani, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limemfukuza kazi meneja wake wa kanda ya Dar es Salaam, Jonas Afumwisye kwa kuzipinga kwenye makundi ya kijamii.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alimwandikia barua Afumwisye kumjulisha kuhusu uamuzi huo Agosti 19 baada ya kuthibitika kwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Afumwisye amekiri kupokea barua hiyo juzi Agosti 22, ila akasema anakusudia kukata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma kama sheria inavyoelekeza.

“Ni kweli nimepata hayo matatizo…utaratibu unaofuata ni kukata rufaa ndani ya siku 45, ” alisema Afumwisye alipoulizwa.

Barua hiyo inaeleza kuthibitishwa kwa tuhuma za Afumwisye kwenda kinyume na kanuni ya 42 jedwali la kwanza, sehemu A kipengele cha 10 cha kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.

“Kati ya Julai 10 na Septemba 25 mwaka 2021, kupitia makundi ya kijamii, ulipinga juhudi za Serikali kuanzisha tozo kwenye miamala ya simu,” inasomeka barua ya Kadogosa.

Ofisa huyo pia anatuhumiwa kupinga juhudi za Serikali kuwapa chanjo wananchi kuepuka milipuko ya magonjwa. Kosa jingine Kadogosa amesema ni kukashfu viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kupitia makundi ya kijamii.

“Kutokana na tuhuma zote kuthibitika, bodi ya wakurugenzi wa shirika kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 13(f) cha Sheria ya Reli namba 10 ya mwaka 2017 imeamua ufukuzwe kazi kuanzia Agosti 19, 2022. Endapo hautaridhika na uamuzi huu, unayo haki ya kukata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma ndani ya siku 45 kuanzia tarehe ya kupokea barua hii. Hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 60 ya kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003,” inaeleza barua hiyo iliyosainiwa na Kadogosa.


Kibano ukipinga tozo

Ukiacha kanuni za tozo ya miamala ya simu zilizoanza kutumika Julai 15 mwaka jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesaini kanuni nyingine zilizoanza kutumia Julai mosi zikikata tozo kwenye miamala yote ya kielektroniki, hali iliyozua kelele za wananchi.

Kwa mujibu wa kanuni hizo za Sheria ya Mifumo ya Kitaifa ya Malipo (tozo za miamala ya kielektroniki) za mwaka 2022, mtu yeyote atakayezipinga anastahili adhabu kali.

Kanuni ya 12(1) kinabainisha kwamba “mtu yeyote atakayekiuka masharti ya kanuni hizi anatenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika kulipa faini isiyopungua Sh5 milioni au kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja.

Kifungu kidogo cha (2) kinafafanua bila kujali kanuni ndogo ya (1), iwapo mtu anatenda kosa chini ya kanuni hizi, Kamishna Mkuu anaweza, pale mtu huyo anapokiri kwa maandishi, kuongeza kosa hilo kwa kukusanya kutoka kwa mtu huyo kiasi cha fedha kisichozidi kiasi cha faini iliyowekwa kwa kosa husika.


Wadau wafunguka

Wakitoa maoni yao kuhusu uamuzi wa TRC, wadau wamesema si haki kumfukuza mfanyakazi kwa kutoa maoni yake kuhusu mambo ambayo Watanzania wengine wanayazungumzia kama yeye.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Tumaini Nyamhokya alisema wanapinga kufukuzwa kwa mfanyakazi huyo kwa sababu ni haki yake kutoa maoni.

“Maoni ya mfanyakazi dhidi ya vitu ambavyo anaona havimridhishi ni haki yake ya msingi na sidhani kama kuna mahala vifungu vya sheria vinampa mamlaka mwajiri kumwondoa mfanyakazi kwa kutoa maoni yake hadharani,” alisema Nyamhokya.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema maoni ya mfanyakazi huyo ni sawa na ya Watanzania wengine wanaoguswa na tozo hizo.

“Hiyo tozo inamhusu hata yeye, sio suala la kikazi. Angekuwa amezungumza chochote kuhusiana na mwajiri, sawa lakini hakuna uhusiano wowote kati ya ajira yake na tozo. Hiyo ni haki yake na anapaswa kwenda kutetewa kwenye vyombo vya kisheria,” alisema Olengurumwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema amesikitishwa na kufukuzwa kazi kwa mfanyakazi huyo na kwamba tukio hilo linaonyesha umuhimu wa haki ya uhuru wa kujieleza bila kuvunja sheria.