Ofisi ya Msajili yabariki kusimamishwa kina Mbatia

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumapili Mei 22, 2022, kuhusu vurugu zilizotokeakatika makao makuu ya chama hicho , kulia ni Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini, Mohamedi Tibanyendera. PICHA NA MICHAEL MATEMANGA

Muktasari:

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imeridhia kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia na Sekretarieti yake yote, kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapoamuliwa vinginevyo.

Dar es Salaam.  Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imeridhia kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia na Sekretarieti yake yote, kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapoamuliwa vinginevyo.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Mei 25, 2022 na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza akisema uamuzi wa Kikao cha Halmashauria ya chama hicho kilichofanyika Mei 21 mwaka huu, ulikuwa halali kwa akidi ya wajumbe wake licha ya kutotaja uhalali wa akidi hiyo.

Nyahoza amesema kwa mamlaka ya ofisi hiyo, inamtaka Mbatia kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapotenguliwa na chama.

“Baada ya kusimamishwa, katibu wa chama hicho alituletea barua kwa fomu ya kisheria inayotujulisha kusimamishwa uanachama, tumekubaliana na uamuzi huo. Kama hawataridhika (Kina Mbatia) ziko njia za kutafuta haki, waende mahakamani,”amesema Nyahoza.

Jumamosi Mei 21 mwaka huu, Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi ilimsimamisha Mbatia na makamu Mwenyekiti Bara, Angelina Mtahiwa kutojihusisha na shughuli zozote za chama hadi mkutano mkuu utakapoitishwa ili wajieleze kuhusiana na tuhuma zinazowakabili.

Mbatia na wenzake walisimamishwa kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwamo kugombanisha viongozi na hivyo kulazimisha kujiuzulu.

Hata hivyo, Siku moja baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi kutangaza kuwasimamisha viongozi hao, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya chama hicho ilikutana na kutoa maazimio manne likiwamo la kuwasimamisha nafasi za uongozi Makamu mwenyekiti Zanzibar, Ambar Hamid, mweka hazina, Suzan Masele na naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Amer Mshindan.

Akisoma maazimio hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la chama hicho, Mohamed Tibanyendela alisema wamewasimamisha viongozi hao hadi pale Halmashauri Kuu itakapokutana.

Tibanyendela alisema maazimio mengine ni kutotambua mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika Mei 21 kutokana na kutokuwapo kwa mujibu wa Katiba ya chama chao.

Pia, alisema Kamati Kuu imelaani Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia migogoro ya chama na tayari wameshamuandikia barua pamoja na mamlaka yake ya uteuzi.

Azimio jingine ni kutoitambua bodi ya wadhamini iliyoteuliwa kwa madai kuwa bodi hiyo ipo kihalali na inaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa NCCR, Mbatia alisema chama hicho ndicho muasisi wa mageuzi Tanzania, hivyo wanaamini katika mwafaka wa kitaifa.

Amesema mambo yaliyotokea ni changamoto ndogo sana, hivyo wanaamini watazisimamia.