Othman akumbusha mshikamano akitambuliwa kwa wanachama

Saturday May 29 2021
othmanpic
By Haji Mtumwa

Unguja. Mjumbe  wa  kamati kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, Othman  Masoud  Othman  amewataka  wanachama wa chama  hicho  kushikamana  ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa ikiwamo ya kudumisha umoja.

Othman ambaye pia ni makamu wa kwanza wa rais Zanzibar ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Mei 29, 2021 Wilaya ya Kaskazini A Unguja katika kikao cha kumtambulisha kwa viongozi na wafuasi wa chama hicho.

Amebainisha kuwa umoja na  mshikamano uliopo katika chama hicho ndio uliokipa nguvu  na  heshima   Zanzibar  na Tanzania Bara.

“Wazee  wetu  walisema  umoja  ni  nguvu  na  utengano  ni  udhaifu, mshikamano huo ndio uliopelekea uimara wa chama. Kwa sababu  ya  mshikamano  wetu  hatuyumbi katika  kudai haki pamoja na  mamlaka  ya Zanzibar  ndani  ya  Tanzania  na  nje  ya Tanzania, ”amesema Othman.

Huku akieleza jinsi wanaojiunga na chama hicho wanavyovutiwa na mshikamano wao, Othman amewataka wanachama wa ACT-Wazalendo kutouchezea mshikamano huo huku akiwataka kuenzi yaliyofanywa na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.

“Tunalopigania  tuendeshe  nchi  yetu  kistaarabu pasina mtu  yoyote  kupata  madhara  wakati  wa uchaguzi  na baada  ya  uchaguzi kwani tuna haki ya  kuishi  kwa  amani  katika  nchi  yetu.” Amesema.

Advertisement

Akimtambulisha Othman, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji amesema, “leo ninakutambulisha kwa viongozi  wa  mikoa  ninachokuomba  usikae  nyuma  tuanze  kazi  ya  kujenga  chama  na kupigania  haki za Wazanzibari.”


Advertisement