Othman: Takwimu za sensa zitumike katika mipango ya maendeleo

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya akimkabidhi ripoti ya matokeo ya sensa ya mwaka 2022 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud ofisini kwake Migombani Zanzibar.

Muktasari:

  • Katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina jumla ya watu milioni 61.74 huku Zanzibar ikiwa na watu milioni 1.8.

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud amesema iwapo taarifa za sensa zikitumika vyema zitaleta tija katika kuratibu na kusimamia utekelzaji wa mipango ya maendeleo nchini.

Ameoa kauli hiyo leo Juni 7, 2023 ofisini kwake Migombani Zanzibar wakati akipokea ripoti ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, kutoka kwa wajumbe wa kamati maalumu ya takwimu Zanzibar.

Ujumbe huo uliongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya, Kamisaa wa sensa Nchini, Balozi Mohamed Hamza na Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, Salim Kassim Ali.

“Kama ambavyo zoezi hilo lilivyofanyika kwa ufanisi wa hali ya juu kutokana na teknolojia ni fursa kwa watendaji na wasimamizi wa taasisi za Serikali kutumia taarifa hizo katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo,” amesema

Amesema sehemu kubwa ya utajiri katika ulimwengu wa sasa upo katika takwimu.

Amesema ni muhimu pia katika matumizi ya takwimu sekta binafsi kushirikishwa kikamilifu ili kusaidia muamko wa matumizi ya taarifa muhimu na kuhamisha ushiriki wa maendeleo kwa jamii.

Naye Dk Saada amesema kuna kazi nzito ya kuihusisha na kuijengea uelewa jamii kwa upana kuhusu umuhimu wa taarifa za sensa katika maendeleo na maisha na katika kulizingatia hilo katika hotuba yake yake ya bajeti ya mwaka wa Fedha wa 2023/24 itakayosomwa hivi karibuni imelizingatia.

Kamisaa wa Sensa, Balozi Mohamed Hamza, amesema usambazaji wa tarifa za sensa umeanzia ngazi za kitaifa lakini utapelekwa hadi kwenye ngazi za chini za shehia na mitaa ili kuleta matokeo chanya.