Pacha Eliud na Elikana katika changamoto mpya

Watoto pacha waliotenganishwa mwaka 2013 nchini India, Elikana na Eliud Mwakyusa (10) wakiwa na wazazi wao Erick Mwakyusa na Grace Joel, nyumbani kwao Boda, Kyela mkoani Mbeya. Picha na Rajabu Athumani

Kyela. Licha ya kuonekana wenye afya njema, Elikana na Eliudi Mwakyusa (10) maisha yao baada ya kutenganishwa hayajawahi kuwa sawa kwao kutokana na kushindwa kuzuia haja kubwa na ndogo

Pacha hao wanashindwa kuzuia kwa kuwa hawaihisi pindi wanapotaka kujisaidia, changamoto hiyo inawanyima kujiamini na kushiriki masomo vizuri kama watoto wengine.

Pacha hawa waliozaliwa Februari 20, 2013 wakiwa wameungana huku wakitumia njia moja kujisaidia, walitenganishwa kwa mafanikio makubwa nchini India na sasa ni wavulana wakubwa wanaosoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Lubele wilayani Kyela, Mkoa wa Mbeya.

Kutokana na changamoto waliyonayo, mara kadhaa Elikana na Eliudi hulazimika kuacha masomo darasani na kurudi nyumbani baada ya kujisaidia, kwani licha ya kuvishwa pampers haja kubwa hutoa harufu inayowafanya wenzao wawatenge.

Kwa mujibu wa mwalimu wao wa darasa, Christina Kabeta pacha hao wana uwezo mzuri kimasomo lakini wamekuwa wakirudi nyuma kutokana na kukosa vipindi vingi kwa kutohudhuria shule au kurudi nyumbani wanapochafuka.

“Pacha hawa wana wakati mgumu, hali inayoshusha uwezo wao, lakini wako vizuri sana kichwani, naamini wanashindwa kutokana na changamoto waliyonayo. Wanaweza kukaa na wenzao ukasikia, “mwalimu, amejititia”, kidogo unaona wanajisikia vibaya na kweli wanatoa harufu wanafunzi wanasema,” alisema.

Mwalimu Kabeta ambaye amewafundisha watoto hao kuanzia darasa la kwanza, anasema hakuna msaada wowote uliotolewa ili kuhakikisha watoto hao wanasoma vizuri.

Mama wa watoto hao Grace Joel (29), alisema changamoto hiyo inaendelea kukua na katika ukuaji wao hawakuwahi kupata hisia ya kupata haja yoyote.

“Wanaendelea vizuri lakini bado hali yao siyo nzuri, kwa sababu haja ndogo inatoka tu yenyewe na haja kubwa hivyohivyo,” alisema.

Alisema kwa mara ya mwisho walikwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2017 na kufanyiwa tena upasuaji na kutakiwa kurudi miezi sita baadaye lakini muda ulipofika hawakwenda kutokana na kukosa fedha za matibabu na hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili familia hiyo.

Alisema baada ya upasuaji wa awali, watoto hao waliwekewa njia za muda tumboni na baada ya miezi sita walitakiwa kurudi hospitali ambako waliziba na kuanza kutumia njia za kawaida na tangu hapo hali imeendelea hivyo mpaka sasa.

Grace alisema hali hiyo inampa changamoto kubwa katika kuwalea, hasa wanapokwenda shuleni kwani hulazimika kuwavalisha pampers asubuhi na mchana wanaporudi anawavalisha nyingine kwa ajili ya masomo ya mchana, hivyo humgharimu Sh2,000 kila siku.

“Wana miaka 10 wanasoma darasa la tatu. Kama lisingekuwa hili tatizo wangeanza shule mapema na sasa wangekuwa darasa la tano. Walianza shule na miaka saba,” anasema.

Grace anasema licha ya changamoto hizo kuna vyakula ambavyo hawawezi kula ikiwemo mboga za majani kwani huarisha sana, hivyo wanakula zaidi maharage na mboga nyinginezo.

“Kiafya wapo vizuri kama unavyowaona ila changamoto kubwa ndiyo hizi,” anasema Grace huku akiiomba Serikali kusaidia watoto hao warudi kwenye matibabu kama ambavyo madaktari wa India walisisitiza baada ya upasuaji wa kwanza.

“Naiomba Serikali inisaidie kwa changamoto ninayoipata kwa matibabu ili watoto wangu wawe sawa. Siwezi kwenda popote, nashindwa kuwaacha peke yao kutokana na hali yao na ninashindwa hata kufanya biashara ili kuwaangalia wao.

“Nikiwepo wakichafuka niwachotee maji waoge, wabadilishe nguo, wazifue nawasimamia maana wameshakuwa wakubwa,” anasema Grace na kuongeza kuwa amewahi kuwasaidia kuwajengea uelewa lakini imeshindikana.

“Nikiamka nawaambia nendeni chooni mkajisaidie, wanarudi wakisema “mama hakitoki kitu” baada ya dakika mbili anatembea choo kimeshuka na wanasema hawahisi chochote, wanashtuka tu haja imetoka.”

Grace ambaye kwa sasa ana mtoto mwingine, Erick (3), anasema pacha wake wana uelewa mzuri darasani lakini changamoto ni maumbile waliyonayo ambayo anaamini wanaweza kupatiwa tiba.

Wanahitaji msaada

Daktari mbobezi wa upasuaji wa watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Zaitun Bokhari anasema kutokana na namna walivyokuwa wameungana, walikuwa hawana mfumo uitwao kitaalumu sphincter.

Dk Zaitun ambaye alishiriki upasuaji wa kuwatenganisha nchini India, anasema kutengeneza mfumo huo ni kitu kigumu, hivyo wataendelea kufanya mafunzo ya chooni, kwa kuwa hiyo ni tofauti na kuwekewa njia ya tumboni.

"Kuna njia ya moja kwa moja huwekwa ubavuni colostomy ambayo inakuwa ni rahisi kujisafisha hata akiwa mkubwa, sasa wengine ile ya kuwekewa ubavuni hawaitaki kwahiyo wanaomba kupata choo hukuhuku chini na kwa kuwa ni wadogo ndiyo maana unaona wanajichafua.

"Lakini wakiwa wakubwa wataweza na watabaki wakavu kwa muda wa saa fulani, kisha kikikaribia wanajisafisha. Muda utafika lakini kwa sasa ni mapema mno kusema kwamba tutaweza kurekebisha hilo tatizo," anasema Dk Zaitun.

Hata hivyo, Dk Zaitun anasema pacha hao wanahitaji msaada zaidi ikiwemo bima za afya kwani wamekuwa wakishindwa kuhudhuria kliniki kutokana na uchumi kuwa mgumu.

“Binafsi nimekuwa nikiwasaidia kwa miaka, kwa sasa nipo Saudi Arabia," anasema.

Baba aelemewa

Erick Mwakyusa (39) ambaye ni baba wa watoto hao anasema amekuwa akinunua pampers muda wote na anapokwama kufanya hivyo watoto wake hawawezi kwenda shuleni.

“Tuliambiwa twende Muhimbili mara ya kwanza walifanyiwa marekebisho tukarudi na awamu nyingine tukaenda wakafanyiwa marekebisho kwa ajili ya haja zao, tuliambiwa namna tutakavyowasaidia na kwamba kadri wanavyokua wangerudi kuwa sawa kwa maana wanaendelea kujitambua.

“Kwa sasa wamekua na wana akili lakini tumegundua hakuna mawasiliano wanapotaka kupata haja. Niliambiwa nikate bima lakini nashindwa kipato hakitoshi, ndugu walitusaidia lakini nao sasa wana majukumu mengine,” anasema Mwakyusa ambaye anafanya kazi ya kusafirisha abiria kwa pikipiki maarufu bodaboda.

Hata hivyo, anasema kwa mujibu wa mkewe Grace, madaktari waliagiza watoto hao warudishwe India kuwekewa njia za haja, jambo ambalo anasema halikufanyika na badala yake watoto hao walitibiwa Muhimbili.

“Mke wangu aliniambia hawa watoto wanatakiwa kurudi warekebishwe sehemu zao za haja ndogo na kubwa kwamba wangefanyiwa hukohuko India, lakini tuliishia Muhimbili,” alisema.

Mwakyusa anasema watoto wake hawaumwi wala kuugua hovyo, lakini wanapambana na changamoto hiyo pekee na baadhi ya vyakula.

“Gharama ni kubwa, hapa nimepanga mahitaji yao muhimu huwa natimiza chakula na nini lakini pampers pekee zaidi ya Sh20,000 kwa mwezi sasa sina hakika kama watamaliza darasa la saba na wakati mwingine ninaweza kuingia barabarani na kipato nisipate, wanashindwa kuhudhuria masomo inaniumiza sana.”