Padre akemea wanaoharibu utamaduni wa Watanzania

Muktasari:

  • Waamini wa Parokia ya Bikra Maria Msaada wa Daima iliyoko Kisiwa cha Kome mkoani Mwanza wametakiwa kudumu katika ibada na kulinda utamaduni wa Watanzania.

Buchosa. Viongozi wa dini na wa Serikali wametakiwa kukemea maovu na kulinda utamaduni ambao ni tunu ya Watanzania.

Hayo yamebainishwa leo Aprii 2, 2023 na Paroko wa Kanisa Katoliki parokia ya Bikra Maria Msaada wa Daima, Padre Japhet Masalu kwenye Misa ya Domika ya matawi iliyofanyika Parokia ya Kome iliyoko wilayani Sengerema mkoa wa Mwanza.

Padri Masalu amesema vitendo visivyofaa na vinavyokwenda kinyume na maadili ya Watanzania vinapaswa kuvikemea ili visienee.

Amewataka waamini kutumia kipindi hiki cha Kwaresima kusali na kumtumaini Mungu.

Katika misa hiyo, Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo amekabidhi tani tano za saruji kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa hilo, akisema ni ahadi aliyoitoa wakati alipofanya harambee ya kuchangia ujenzi wa parokia hiyo.

Shigongo amesema aliona ni vema kutumia ahadi yake aliyoitoa ya kulitumikia Kanisa.

Amewaahidi waamini wa Parokia hiyo atashirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kulijenga Kanisa la Mungu.