Padri Kitima: Vijana watakuja kufanya mapinduzi

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima amesema vijana watakuja kufanya mapinduzi endapo wanasiasa wasipojirekebisha katika mfumo wao wa maisha ya kisiasa.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima amesema vijana watakuja kufanya mapinduzi endapo wanasiasa wasipojirekebisha katika mfumo wao wa maisha ya kisiasa.

Padre Kitima ameyasema hayo jana Alhamisi Septemba 15, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la maadhimisho ya siku ya kimataifa ya demokrasia ambayo iliwakutanisha wadau mbalimbali kujadili miaka 30 ya demokrasia ya Tanzania.

Amesema vijana sasa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa ajira, jambo ambalo linawaongezea hasira za maisha.

“Msipojirekebisha nyinyi wanasiasa, vyama vyote, vijana watakuja kuleta mapinduzi miaka 10, 20 ijayo, hamtayakwepa. Hawana kazi, mnawaibia kura, mnawayumbisha.

“Wameamua kukaa kimya kwa sababu wameamua kutuheshimu sisi wazazi wao na viongozi wao lakini hawatavumilia milele,” alisema Padre Kitima.

Padre Kitima amesema nchi hii inakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na taasisi imara za demokrasia kuanzia kwenye familia, kwenye ukoo, kwenye kijiji hadi kuingia kwenye siasa.

“Tanzania tuna kazi kubwa ya kujenga zile democratic habits (tabia za kidemokrasia) ili watu wafanye kazi zao na kuwaletea wananchi maendeleo.

“Vyama vya siasa tuungane kutengeneza taasisi za kidemokrasia zinazoheshimiwa na watu. Hizo zitatusaidia kujenga tabia za kidemokrasia,” alisema Padri Kitima.

Kwa upande wake, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema viongozi wa dini ni wahusika wakubwa wa demokrasia, hivyo alitaka warudishiwe hadhi yao kwa kuwatambuliwa majukumu yao bila kusema wanajihusisha na siasa.

“Tuna kazi kubwa Tanzania ya kujenga tabia za kidemokrasia ili watu wafanye kazi zao na kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Sheikh Ponda.