Padri kortini kwa mashtaka 178, lipo la kuongoza genge la uhalifu
Muktasari:
- Washtakiwa wawili, akiwemo Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bunda mkoani Mara, Karoli Mganga wamefikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa mashtaka 178, likiwemo la kuongoza genge la uhalifu.
Musoma. Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bunda mkoani Mara nchini Tanzania, Karoli Mganga amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma akikabiliwa na mashtaka 178, likiwemo la kuongoza genge la uhalifu.
Mbali na padri huyo, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni aliyekuwa mhasibu wa kanisa hilo Jimbo la Bunda, Gerald Mgendigendi.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumanne Agosti 6, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Aloyce Katemana na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Akiwasomea mashtaka hayo, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Mara, Amoscsye Erasto amedai walitenda kosa la kughushi nyaraka, kinyume na sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.
Amedai washtakiwa hao wakiwa watumishi wa kanisa hilo, waliiba fedha Sh1.7 bilioni pamoja na fedha za kigeni, ikiwepo Dola zaidi ya 100,000 na Euro zaidi ya 20,000.
Amedai jumla wanakabiliwa na mashtaka 178, yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, utakatishaji fedha pamoja mashtaka mengine mengi.
Hata hivyo, baada ya kusomewa mashtaka hayo hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Kesi itatajwa tena Agosti 20, 2024 na washtakiwa wamepelekwa rumande.