Panda shuka ya viongozi wateule

Panda shuka ya viongozi wateule

Muktasari:

  • Miaka mitano iliyopita ilikuwa ya milima na mabonde kwa Alphayo Kidata ambaye amekuwa akitumikia kila jukumu analopangiwa bila uhakika wa kukaa hapo kwa muda mrefu.

Dar es Salaam. Miaka mitano iliyopita ilikuwa ya milima na mabonde kwa Alphayo Kidata ambaye amekuwa akitumikia kila jukumu analopangiwa bila uhakika wa kukaa hapo kwa muda mrefu.

Sasa amerudi katika nafasi yake ya mwonzani mwa utawala wa awamu ya tano, ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Nafasi hiyo aliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan juzi, haitakuwa ngeni kwake kwa sababu aliwahi kufanya kazi katika mamlaka hiyo akitokea kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Desemba 2015.

Uteuzi uliofanywa na Rais Samia juzi ni kama umemuibua upya Kidata ambaye amepitia milima na mabonde katika utumishi wake serikalini katika miaka takribani sita iliyopita.

Machi 25, 2017, Hayati Rais John Magufuli alimhamisha Kidata kutoka TRA kwenda kuwa Katibu Mkuu Ikulu, nafasi ambayo alidumu nayo mpaka Januari 10, 2018 alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada alikokaa kwa takriban miezi 10.

Novemba 2018, Magufuli alitengua uteuzi wa Kidata na kumrejesha nchini. Katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wakati huo, Dk Faraji Mnyepe, ilisema Rais alimwondolea pia hadhi ya ubalozi.

Septemba 20, 2019, Kidata aliteuliwa na Magufuli kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, nafasi ambayo ameitumikia mpaka juzi alipopata uteuzi mpya katika serikali ya awamu ya sita -- kurejea TRA akiwa Kamishna Mkuu.

Si huyo tu alipepanda milima na mabonde, Rais Samia jana alitengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya petroli Tanzania (TPDC), Thobias Richard ikiwa ni chini ya saa 12 tangu alipomteua.

Juzi Aprili 4, 2021 usiku, Samia alimteua Richard miongoni mwa wakuu wa mashirika ya umma aliowateua lakini ghafla jana asubuhi lilitolewa tangazo la kutenguliwa kwake na kumrejesha kwenye nafasi hiyo aliyekuwa mkurugenzi mkuu, James Mataragio.

Mataragoa naye anayeingia katika rekodi ya waliopanda milima na mabonde kwa kuwa Agosti, 2016, alisimamishwa kazi na Bodi ya TPDC baada ya kuitumikia nafasi hiyo kwa miaka miwili tangu alipoteuliwa na Rais wa wakati huyo, Jakaya Kikwete Desemba 15, 2014.

Dk Mataragio alikuwa akituhumiwa kwa rushwa katika sakata la zabuni, yeye na wakurugenzi wengine katika shirika hilo na alifikishwa mahakamani Machi 2018 kwa kosa hilo.

Lakini Julai 22, 2019 Rais Magufuli aliagiza Wizara ya Nishati kumrejesha kazini mara moja katika nafasi hiyo mtaalamu huyo wa miamba na hatua iliyofuatwa ni kufutiwa kesi zake mahakamani.

Mteule mwingine anayeingia katika kundi hilo ni Profesa Godius Kahyarara, aliyeteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Uwekezaji.

Magufuli alimteua msomi huyo wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Oxford, Machi 16, 2016 akimtoa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumpa Ukurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya jamii (NSSF) akichukua nafasi ya Ramadhan Dau ambaye aliteuliwa kuwa balozi.

Hata hivyo, miaka miwili baadaye (Julai 14, 2018), Rais Magufuli alitengua uteuzi wake na kumteua William Erio ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF kuwa Mkurugenzi mpya wa mfuko huo unaosimamia sekta binafsi.

Baada ya hapo, kimya kilitawala kuhusu Profesa Kahyarara hadi juzi alipoteuliwa na Rais Samia kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Uwekezaji.

Akizungumzia kupanda na kushuka kwa wateule hao, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Frank Tily alisema “pengine Rais ameangalia mafaili ya wateule wake na kuona wanafaa kusaidia maendeleo ya Taifa licha ya kuwa hawakuwa katika nafasi hizo kwa kipindi fulani.

“Ameona kuendelea kuwa pembeni kwao ni kupoteza nguvu kazi muhimu. Rais ameona ni watu wenye uwezo wa kufanya kazi,” aliongeza Dk Tily.