Panga la Rais Samia balaa

Panga la Rais Samia balaa

Muktasari:

Panga la Rais Samia Suluhu Hassan ni balaa. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kiongozi mkuu huyo wa nchi kupangua makatibu wakuu wa wizara, naibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali huku baadhi wakihamishwa.


Dar es Salaam. Panga la Rais Samia Suluhu Hassan ni balaa. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kiongozi mkuu huyo wa nchi kupangua makatibu wakuu wa wizara, naibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali huku baadhi wakihamishwa.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amepangua wakuu wa taasisi za Serikali wakiwemo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF) huku akiwagusa makatibu wakuu wa wizara nyeti, ikiwemo ya Fedha na Mipango.

Uteuzi huo umekuja zikiwa zimepita siku tatu tangu kiongozi huyo kutamka kuwa atafanya mabadiliko ya makatibu wakuu, kauli aliyoitoa wakati akiwaapisha mawaziri na naibu mawaziri Alhamisi iliyopita Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma huku akieleza kuwa, huenda kesho (Jumanne) watu wakarejea tena Ikulu katika hafla ya kuapishwa wateule wengine.

Katika uteuzi huo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amehamishiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara.

Pia, Dk Hassan Abbas amebaki kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo lakini nafasi yake ya Msemaji Mkuu wa Serikali ameteuliwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa na hivyo kufanya nafasi hiyo kuwa wazi kwa sasa.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amewaondoa waliokuwa wakuu wa taasisi za Serikali akiwemo Mkurugenzi wa TPA, Deusdedit Kakoko ambaye amesimamishwa kupisha uchunguzi, sasa nafasi yake ameteuliwa Erick Hamis.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi pia ameigusa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kumteua Alphayo Kidata kuwa Kamishna Mkuu kuchukua nafasi ya Edwin Mhede huku TCRA akiteuliwa Dk Jabir Kuwe kuchukua nafasi ya James Kilaba.

Katika uteuzi huo Mganga Mkuu wa Serikali ni Dk Aifello Sichwale, huku Gerald Musabila akiteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Masha Mshombo ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF akichukua nafasi ya William Erio, ambaye taarifa hiyo haikusema kama atapangiwa kazi nyingine ama la huku Kaimu Mkeyenge akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Meli Tanzania (Tasac) na Thobias Richard kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

Awali, nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na James Mataragio ambaye kama ilivyo kwa wengine taarifa haikueleza zaidi kuhusu hatma yao.

MABADILIKO WIZARA

Ujenzi na Uchukuzi:

Katibu Mkuu ni Joseph Malongo na naibu wake ni Gabriel Migire.

Wizara ya Nishati

Katibu Mkuu ni Leonard Masanja na naibu wake ni Kheri Mahimbali.

Maliasili na Utalii

Dk Allan Kijazi amepanda kutoka naibu katibu mkuu kuwa katibu mkuu wa wizara hiyo huku nafasi yake akiteuliwa Ludovick Nduhiye.

Mawasiliano na Teknolojia

Dk Zainab Chaula na naibu wake ni Jim Yonazi.

Katiba na Sheria

Katibu mkuu amebaki Profesa Sifuni Mchome na naibu wake ameendelea kuwa yule yule, Dk Amon Mpanju.

Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Katibu mkuu ni Faraj Mnyepe.

Mambo ya Nje

Katibu Mkuu ni Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na naibu ni Balozi Fatma Rajab.

Mambo ya Ndani:

Katibu Mkuu ni Christopher Kadio na naibu wake ni Ramadhani Kailima.


Madini

Katibu Mkuu ni Simon Msanjila.


Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Katibu Mkuu ni Mary Makondo na Nicholas Mkapa anakuwa naibu wake.

Wizara ya Maji

Katibu Mkuu ni Anthony Sanga na naibu wake ni Nadhifa Kemikamba

Elimu, Sayansi na Teknolojia:

Katibu Mkuu ni Dk Leonard Akwilapona manaibu wake ni Profesa James Mdowe na Dk Carolyne Nombo.

Wizara ya Afya

Katibu Mkuu ni Dk Abel Makubi na naibu wake ni Dk John Jingu

Wizara ya Kilimo:

Katibu Mkuu ni Andrew Massawe na naibu wake ni Profesa Siza Tumbo.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Katibu Mkuu ni Dk Rashid Tamatamah huku manaibu wake.


Wakuu wa mikoa kitanzini

Wakati presha ya makatibu wakuu na watendaji wa taasisi za Serikali ikishushwa jana usiku kwa uteuzi huo, kivumbi sasa kinabaki kwa wakuu wa mikoa na wilaya ambao, zamu yao ndio iko njiani.

Habari ambazo Mwananchi limepenyezewa ni kwamba, huenda baada ya kumaliza kuwaapisha wateule wapya, Rais Samia anaweza kugusia uwezekano wa uteuzi mwingine ambao utahusu wakuu wa mikoa na wilaya kama alivyofanya wakati akiwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri kwenye Ikulu ya Chamwino.