Pangani kutangaza utalii

Muktasari:

  • Wilaya ya Pangani imetakiwa kuweka mkakati maalum kwa kutangaza vivutio vya utalii vya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Utalii wa Bahari.



Pangani. Wilaya ya Pangani imetakiwa kuweka mkakati maalum kwa kutangaza vivutio vya utalii vya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Utalii wa Bahari.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Juni 22, 2022 na Balozi wa Utalii ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Malima amesema wilaya hiyo ina fukwe nzuri pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Saadani lakini haitangazi fursa zilizopo.

"Mimi ni balozi wa utalii sasa baada ya wiki tatu nakwenda kuweka kambi Saadani na waandishi kwa nia ya kutangaza hifadhi hii na ninataka mniunge mkono.

"Wilaya ya Pangani inapakana na Hifadhi ya Saadani lakini Pangani mmelala hamuoni kama ni fursa kwenu barabara ikikamilika tukifanya matangazo mahoteli yatajengwa Pangani watu walala hapa na watakwenda kufanya utalii Saadani hamuoni kama hii ni fursa ndugu zangu tuchangamke," amesema Malima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Hamashauri ya Pangani, Akida Baholera amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa huyo kwamba Baraza la Madiwani kwa kushirkiana na watumishi watamuunga mkono kwa kuhakikisha wanaitangaza Hifadhi ya Saadani.