Panyabuku waanza kutumika kubaini TB Tanzania

Friday February 26 2021
panyapic

Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Abel Makubi akiwa amembeba panyabuku aitwae Justin ambaye alitumia dakika tano kubaini sampuli 6 za vimelea vya kifua kikuu kutoka katika makohozi 60. Profesa Makubi ametembelea mradi wa Apopo unaofundisha panya hao kubaini vimelea vya Kifua kikuu katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kilichopo Morogoro.

By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imeshaanza kutumia teknolojia ya Panyabuku katika kubaini ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa sampuli za wagonjwa wenye dalili hizo.

Mchakato huo umekuja ili kuongeza uwezo wa kutambua vimelea hivyo hasa pale ambapo njia nyingine zimeshindwa.

Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Abel Makubi ambaye alitembelea kitengo hicho cha APOPO katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Morogoro amepongeza mapinduzi kutoka kwa Wanasayansi ya kuwawezesha panya buku wa Chuo Kikuu hicho kunusa na kubaini vimelea vya Kifua Kikuu.

Panya hubaini kupitia sampuli za makohozi yanayoletwa hapo kwa ajili ya vipimo vya Kifua Kikuu, na  ameelekeza kufikia mwaka huu huduma hiyo iweze  kuzifikia zaidi ya Hospitali 100 nchini.

Profesa Makubi amesema Panya hao wana uwezo mkubwa wa kugundua vimelea vya Kifua Kikuu hata kwa mtu ambaye alifanya vipimo Hospitalini kama vile vya hadubuni (microscope) na mashine za kupima vinasaba mfano GeneXpert na vipimo vingine na vikatoa majibu kuwa hana TB, lakini panya hao wana uwezo wa kubaini vimelea ambavyo mashine za hospitalini zinaweza zisibaini.

“Hii inaonyesha utumiaji wa panya hawa unaweza kusaidia kuongeza ugunduzi wa wagonjwa wengi zaidi. Panya mmoja ana uwezo wa kugundua kama sampuli ina vimelea vya kifua kikuu kwa muda wa sekunde moja, na hupima sampuli za makohozi 100 kwa dakika 20 hivyo teknolojia hii inaweza kutumika hata kwenye upimaji wa sampuli nyingi kutoka kwenye kundi kubwa la watu (mass Screening) kwa muda mfupi.” Amesema Profesa Makubi.

Advertisement

Mganga Mkuu wa Serikali alishuhudia Panya ajulikanae kwa jina la Justine aliyepima sampuli 60 za makohozi ndani ya dakika tano na kugundua sampuli sita zenye vimelea vya Kifua Kikuu.

Mpaka sasa huduma hiyo inatolewa katika hospitali 74 na kubaini wagonjwa 14,680 ambao hawakugundulika kwa njia za kawaida.

 Hii imesaidia wagonjwa 8,119 kuanza matibabu ambayo yamezuia maambukizi ya kifua kikuu kwa wanachi 81,190 hadi 121,785 ambao wangekuwa hatarini kuambukizwa kutokana na mgonjwa mmoja ambaye hajatibiwa anaweza kuwaambukiza watu 10 hadi 15 walio karibu naye kwa mwaka.

Advertisement