Pete inavyozuia VVU kwa wanawake

Muktasari:

Wakati wataalamu wakiendelea na utafiti wa dawa ya kutibu ukimwi, imegundilika mbinu mpya ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa wanawake kwa kutumia pete maalumu iitwayo ‘Dapivirine Vaginal Ring’.


Dar es Salaam. Wakati wataalamu wakiendelea na utafiti wa dawa ya kutibu ukimwi, imegundilika mbinu mpya ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa wanawake kwa kutumia pete maalumu iitwayo ‘Dapivirine Vaginal Ring’.

Pete hiyo ambayo inapewa nafasi kubwa ya kushusha maambukizi kwa kundi hilo, ina madini ya silikoni inayovaliwa ukeni na hudumu kwa siku 28 na hutoa dawa kinga ya ‘dapivirine’ inayoua virusi vya ukimwi ukeni.

Imeelezwa kuwa ni rahisi kuivaa, inakinga virusi kwa asilimia kubwa na hata mwenza hawezi kubaini iwapo mwanamke ameivaa.

Ujio wa pete hiyo umetokana na utafiti wa muda mrefu uliolenga kutafuta njia ya kuwalinda wanawake dhidi ya maambukizi ya VVU wakati wa kujamiiana bila kutegemea wanaume kuvaa mipira (kondomu).

Kinga hiyo imekuja baada ya utafiti wa miaka zaidi ya 10 kufanyika nchini Marekani na Afrika na mwaka 2020 Shirika la Afya Duniani (WHO) liliruhusu pete hizo kutumika kama njia ya kinga na mpaka sasa nchi nne zimeanza kutumia ikiwemo Afrika Kusini, Uganda, Zimbabwe na Malawi.

Kwa upande wake, Serikali imekiri kuifuatilia pete hiyo na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale alipoulizwa alisema Wizara ya Afya ina taarifa na uwepo wa kinga hiyo mpya.

“Taarifa pia zimepokelewa kupitia asasi zisizo za kiserikali (CSOs) pamoja na umoja wa wanawake wanaoishi na maambukizi ya VVU wakihimiza upatikanaji na matumizi ya dawa yaanze.

“Wataalamu wizarani kupitia NACP (Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi) watashirikiana na Taasisi ya utafiti na TMDA (Mamkala ya Dawa na vifaa tiba) kuendelea na mjadala kuangalia ubora na usalama wa dawa hiyo kabla ya kuanza kutumika nchini na kama ina faida zaidi ukilinganisha na kinga za aina nyingine zinazotumika,” alisema.

Dk Sichwale alisema nchi nyingi bado zinafanya majiribio na matokeo yatatoa mwanga na mapendekezo katika kutumia aina hiyo ya kinga, kwani WHO ilipanga kukaa kikao cha wataalamu kujadili dawa hiyo na Aprili 28, mwaka huu imepitisha dawa hiyo itumike.

“Hadi sasa nchini dawa hii haijawekwa kwenye utaratibu wa manunuzi na upatikanaji. Pale tutakapokuwa tumetekeleza na kuwa na tathmini halisi ya utumiaji wa afua kinga ya PrEP ambayo imeanza kutekelezwa Novemba 2021, tathmini itatoa mwelekeo wa kuongeza au kutoongeza aina nyingine ya dawa,” alisema Dk Sichwale.


Pete inavyotumika

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Dare, Dk Lilian Mwakyosi alisema pete hiyo itakuwa mkombozi kwa wanawake na wasichana walio katika hatari ya kuambukizwa VVU.

“Hii ni njia mpya ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi tofauti na njia nyingi ambazo tumekuwa nazo kwa muda mrefu. Pete huvalishwa ukeni na hutoa dawa kinga ambayo ni aina fulani ya ARV inayofanya kazi kama vidonge vya Pre-Exposure Prophylaxis (PrEP) yenye uwezo wa kuzuia maambukizi ya VVU ikiwa mtumiaji atameza kila siku kwa siku saba kabla hajashiriki tendo na kuendelea kuitumia kila siku.

“Pete hiyo mpya ina uwezo wa kukinga maambukizi dhidi ya VVU kwa asilimia 99, lakini yenyewe inazuia maambukizi kwa njia ya ukeni tu,” alifafanua.

Dk Mwakyosi alisema pete hiyo imetengenezwa kwa silicone ambayo inakuwa rahisi hata kuivaa na ni njia ya muda mrefu, kwani watu wana uhitaji tofauti.

“Si kila mtu anaweza kutumia PrEP kumeza kidonge kila siku. Kuna kujisahau au kuvaa kondomu wakati wote. Dawa hiyo itawafanya wanawake wafanye chaguo lipi linamfaa zaidi,” alisema.

Pete hiyo iliyotengenezwa na shirika la kimataifa la dawa za viumbe hai International Partnership for Microbicides (IPM) waliojikita kutengeneza njia mpya ya kuzuia maambukizi ya VVU nchini Afrika Kusini, mwaka 2019 ilithibitishwa rasmi kwamba inaweza kutumika.

Mwaka 2020, WHO iliiruhusu rasmi itumike kama njia mojawapo ya kujikinga dhidi ya VVU. Hata hivyo, Tanzania kwa sasa bado inatumia kondomu na PrEP kama njia kinga dhidi ya VVU.


Kuhusu pete

Dk Mwakyosi alisema kazi yake si kuondoa matumizi ya kondomu kwa wanaume, bali kuzuia maambukizi ya VVU kwa njia ya uke pekee.

“Hii inamaanisha matumizi ya kondomu yanabaki palepale, kondomu bado ni muhimu kwa kuwa inazuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa, mimba zisizotarajiwa na hata saratani ya shingo ya kizazi.

“Ivaliwe kwa siku 28, hairuhusiwi kuitoa labda uwe umeongea na mtoa huduma za afya, labda kama ataona kuna changamoto ataruhusu itolewe,” alisema.

Hata hivyo, alisema ni muhimu kuhakikisha anapima magonjwa ya ngono mara kwa mara kwa kuwa ni rahisi mtu kujisahau na kutotumia kondomu, inaweza kuwa si salama akapata magonjwa ya ngono wakati amevaa pete, ikiwa hivyo inaongeza hatari ya kupata maambukizi.

Pia alisisitiza kuwa kuzidisha siku 28 inapunguza ufanisi wa kifaa hivyo, kivaliwe ndani ya siku sahihi tu.

“Hiki kifaa ni laini na kinakunjika, mwanamke ataikunja petekatika umbo la namba 8, ni rahisi na kuna mkao akae aiingize na ataisaidia kuisukuma kwa kidole iweze kuingia.

Inachukua muda mfupi inakaa vizuri kwa kuwa inakwenda kukaa kwenye mlango wa kizazi na haina kero yoyote kwa mtumiaji,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu maudhi madogo madogo alisema: “Mpaka sasa hakuna ripoti yoyote kwa waliotumia kuonyesha wamepata madhara na kwamba, ni kubwa hivyo si rahisi kupenya kwenye shingo ya kizazi.


Umuhimu wake

Hapa nchini wasichana wadogo na wanawake wengi wamekuwa wakifanya ngono zembe wakiamini dawa za dharura za kuzuia ujauzito ‘Emergence Contraceptive Pills’ maarufu P2 na kutozingatia matumizi ya kondomu, hali inayowaweka katika hatari ya kupata virusi vya ukimwi na magonjwa mengine.

Wataalamu wanasema uwepo wa pete hizo utasaidia kundi kubwa la wanawake wanaoathirika kwa kupata maambukizi mapya ya VVU ambapo, takwimu zinaonyesha wasichana 80 wenye umri wa miaka 15 mpaka 25 wanaambukizwa VVU kila siku.

Dk Mwakyosi alisema kwa mara ya kwanza kuna njia ya muda mrefu na kumwezesha mwanamke kujilinda bila kushirikisha upande wa pili na hiyo itasaidia kupunguza changamoto.

“Tunaziongelea kila siku, hasa kwa wasichana balehe moja ya changamoto ni kukubaliana matumizi ya kondomu na wenza wao. Ni muhimu ifike ikubalike mapema kwani maambukizi hayasubiri,” alisema.

Veronica Lyimo kutoka Jukwaa la wanawake wanaoishi na VVU Tanzania alisema kinga hiyo ni muhimu kwa wanawake kwa kuwa, itapunguza maambukizi kwa waliopo hatarini.

“Baadhi ya nchi wameikubali hii pete na imewasaidia wanawake wengi. Shuhuda zipo nyingi, ili kujikinga kuna haja ya kuwa na vitendea kazi tofauti ibaki kwa mwanamke achague ni aina ipi atumie kama ni sindano, kutumia kondomu au kuvaa pete ukeni ambayo itamsaidia yule asiye na maamuzi kutumia ili asipate maambukizi,” alisema Veronica.

Wasikie waliotumia

Mkazi wa Cape Town nchini Afrika Kusini, Akhona Gxarhisa (27) ni miongoni mwa wanawake walioshiriki katika utafiti huo ambaye aliisifia kuwa ni nzuri.

“Nimefurahi kuwa sehemu ya wanawake waliookoa wanawake wengine, ninahisi mimi ni shujaa,” alisema Gxarhisa.

Kwa takriban miaka mitano, Akhona alikuwa na pete ya uke bila matatizo, huku mwenza wake wa wakati huo alikuwa na maambukizi na yeye kuwa sehemu ya majaribio.

“Kwangu, mwenzangu hakuhisi nina kitu hiki ndani mpaka nilipomwambia.”

Mwanamke mwingine aliyeshiriki katika utafiti huo alisema kwa miaka mitatu mwanamume aliyekuwa naye ‘mwenye maambukizi’ hakufahamu kama ana pete, lakini baada ya kumwambia alisema anaihisi, hivyo lazima aitoe. “Nilipokataa aliniacha,” alisema.


Msimamo wa nchi

Machi 11, mwaka huu, Afrika Kusini waliruhusu pete hiyo kutumika na wanawake, wakati Zimbabwe ilikuwa nchi ya kwanza kuruhusu kinga hiyo mwaka 2021.

Mpaka sasa nchi zilizolengwa kutumia pete hizo kupunguza maambukizi kwa wanawake ni Eswatini, Kenya, Lesotho, Malawi, Rwanda, Afrika Kusini, Uganda, Zambia na Zimbabwe.


Makundi ya hatari

Makundi yaliyo katika hatari ni pamoja na wasichana wenye umri kuanzia miaka 15 mpaka 25, kinamama wadogo, wafanyabishara wa ngono, wanawake walio katika ndoa zisizo na uaminifu na waishio na wenza wenye maambukizi.

Maambukizi ya VVU yanaenea kwa kasi zaidi kwa kundi la wasichana balehe wenye umri wa miaka 15 hadi 24 kwa asilimia 2.1, ikiwa ni mara tatu zaidi ya vijana wa kiume kwa asilimia 0.6.

Kwa mujibu wa wataalamu, wasichana wawili mpaka watatu wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 24 huambukizwa VVU kila baada ya saa moja hapa nchini.

Meneja wa Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi Tanzania (ATF), Peter Kivugo alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita zaidi ya watu 200 wamekuwa wakiambukizwa virusi vya ukimwi kila siku, huku asilimia 40 ikiwa wasichana wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 25.

Idadi hiyo ni sawa na wasichana 80 kwa siku, ambapo wengi wamekuwa wakifanya ngono zembe wakiamini P2 zitawakomboa na kuweka kando matumizi ya kondomu. Pia, hali hiyo inawaweka kwenye hatari ya kupata maambukizi ya ukimwi, homa ya ini, magonjwa ya zinaa, saratani na ugumba.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita zaidi ya watu 200 wamekuwa wakigundulika kuwa na maambukizi ya VVU kwa siku, kati ya hao asilimia 40 ni wasichana wadogo wenye umri wa miaka 15 mpaka 25,” alisema Kivugo.

Ofisa Ufuatiliaji na Tathimini wa Tacaids, Nyangusi Laiser alisema asilimia 60 ya kundi balehe la vijana wa kati ya miaka 15-24 walipima na kujua hali zao kwa mwaka 2020.

Alisema kati ya waviu wapya 68,000 waliokutwa na maambukizi mapya, asilimia 28 walikuwa na umri wa miaka 15 mpaka 24 na kati ya hao asilimia 67 walikuwa wasichana balehe na wanawake vijana huku wavulana wakiwa asilimia 23.

“Wasichana wanaathirika zaidi kutokana na mila na desturi, mimba za utotoni, ngono za mapema, maambukizi ya magonjwa ya ngono, kutokuwa na maamuzi, unyanyasaji wa kijinsia na mengineyo,” alisema.


Hali ya maambukizi

Kwa mujibu wa ripoti ya Juni, 2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi ni asilimia 4.9 (asilimia 6.3 ni wanawake na asilimia 3.4 ni wanaume).

Hata hivyo, Nyangusi alisema maambukizi mapya katika maeneo ya mjini ni asilimia 5.5, huku maeneo ya vijijini ni asilimia 4.2 na idadi ya watu wanaoishi na VVU kufikia Novemba mwaka 2021 ni milioni 1.7.

Alieleza kuwa maambukizi mapya ya VVU kufikia mwaka 2021 yamepungua kufikia 68,000 wakati vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi vikiwa 27,000.

Nyangusi alisema kutokana na afua mbalimbali zinazotekelezwa nchini, idadi ya watu wanaofahamu kuwa wanaishi na VVU ni asilimia 84, asilimia 98 wanatumia dawa za kufubaza virusi (ARVs) na asilimia 92 wanaotumia ARVs wamefanikiwa kuvifubaza virusi hivyo.


Chanjo zingine

Mwaka 2021 matumiani ya kupatikana kwa chanjo ya virusi vya ukimwi yalianza baada ya kampuni ya kutengeneza chanjo ya Moderna ya nchini Marekani kuanza majaribio ya chanjo ya ‘mRNA-1010’ kwa binadamu.

Hatua ya majaribio kwa binadamu ilifuata baada ya kampuni hiyo yenye aina mbili za chanjo za ukimwi kufuzu hatua za awali za kimajaribio na hivyo kuanza kutumika kwa binadamu.

Chanjo zilizopo kwenye majaribio ni pamoja na mRNA-1644 na mRNA-1644v2-Core, ambazo zote zimeshachunguzwa na kufanyiwa majaribio na kuonekana salama kabla ya kujaribiwa kwa binadamu kwa mara ya kwanza.


Tofauti ya pete, PrEP, PEP na ARV

Pete huvaliwa na mwanamke ambaye hajapata VVU na inatoa dawa kinga inayozuia maambukizi kwa njia ya ukeni.

PrEP inapatikana kama vidonge na inapaswa kunywewa kabla ya kujamiiana ili kuepuka maambukizi. Pia hutumika kumkinga mtu na maambukizi ndani ya saa 72 na inaelezwa inapunguza hatari ya kupata maambukizi kutokana na ngono kwa takriban asilimia 99 inapotumiwa kama ilivyoagizwa.

ARV ni kwa ajili ya mtu mwenye maambukizi na anaitumia ili kulinda kinga yake ya mwili isidhoofishwe na virusi.