Polisi akatwa panga akikamata mtuhumiwa

Muktasari:

  • Polisi mkoani Kilimanjaro, wanamsaka mtuhumiwa wa mauaji aliyemjeruhi kwa kumkata kwa panga kichwani, askari wa jeshi hilo, wakati askari huyo na wenzake walipofika nyumbani kwake kwa lengo la kumkamata.


Siha. Polisi mkoani Kilimanjaro, wanamsaka mtuhumiwa wa mauaji aliyemjeruhi kwa kumkata kwa panga kichwani, askari wa jeshi hilo, wakati askari huyo na wenzake walipofika nyumbani kwake kwa lengo la kumkamata.

Askari huyo wa kituo cha Polisi Sanyajuu wilayani hapa, Wilfred Kavishe (pichani) alijeruhiwa kichwani usiku wa Septemba 27 na mtuhumiwa huyo, ambaye ni miongoni mwa watuhumiwa wa mauaji yaliyotokea kijiji cha Naibili.

Siku hiyo, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walimshambulia kwa mapanga mtu aitwaye Serafini Mrama na kufariki dunia wakimtuhumu kumkata ng’ombe wa jirani yake mguu wa nyuma na kuondoka nao kwa ajili ya kitoweo.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Mdogo, alipoulizwa jana na Mwananchi, alithibitisha kutokea kwa tukio la askari huyu kukatwa kwa panga kichwani na kwamba taarifa za kina zitatolewa kesho na kamanda wa Polisi Mkoa, Simon Maigwa.

“Ni kweli hilo tukio lipo na tuna masikitiko makubwa kuwa kijana wetu amejeruhiwa akitekeleza majukumu halali na ya kisheria na walifuata taratibu zote. Njoo Jumatatu (kesho) afande RPC (Maigwa) atakupa taarifa kamili,”alisema.


Madai ya bomu la machozi

Kaimu kamanda huyo alisema Kamanda Maigwa ndiye anayeweza kutolea ufafanuzi wa taarifa za matumizi ya bomu la machozi katika purukushani hizo ambalo inadaiwa lilisababisha uharibifu na kumlazimisha mtuhumiwa kutoka ndani.

Wakati Kaimu kamanda huyo akisema hayo, gazeti hili lilimtafuta askari huyo ambaye alieleza siku hiyo saa 5 usiku walikwenda kumkamata mtuhumiwa, lakini walipofika nyumbani kwa mtuhumiwa, alijifungia ndani na kugoma kutoka.

“Sasa katika kufungua ule mlango ndio alitoa panga na kunikata kichwani ila baada ya muda nyumba ilianza kutoka moshi alitoka na kukimbia ila mke wake alitoka salama,” alisema polisi huyo bila kufafanua moshi huo ulisababishwa na nini.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Naibili, Sebastian Shirima ambaye ana undugu na mtuhumiwa wa shambulizi hilo, alieleza siku hiyo usiku saa 6 alijulishwa kuwa polisi na viongozi wa vijiji, wamefika nyumbani kwa ndugu yake.

Katika mawasiliano hayo, alijulishwa askari hao walikuwa wameambatana na mtendaji wa kijiji hicho pamoja na mwenyekiti wa kijiji. “Ni kweli polisi walifika wakiongozana na viongozi wa kijiji; huyu ndugu yangu naambiwa akamkata kwa panga polisi na katika purukushani hizo kulisikika milio kama wa bomu la machozi lililorushwa ndani ya nyumba,” alidai Mallya.

Mtendaji wa kijiji hicho, Melikiao Patrick, alieleza siku hiyo saa 2 usiku alipigiwa simu na polisi muda wa saa mbili usiku kwamba wanakwenda kijijini kwake kwa ajili ya kuwatafuta washukiwa kadhaa wa tuhuma za mauaji.

“Baada ya hapo tuliongozana hadi katika nyumba ya mtuhumiwa ambapo tulijitambulisha na kumtaka afungue mlango hakufungua ndipo askari alisukuma mlango akakatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na damu nyingi kutoka”alidai.

Mtendaji hiyo alidai baada ya kuona damu, yeye alikimbilia kwenye gari ya polisi na baadaye ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo alifanikiwa kutoroka na hivyo Jeshi la Polisi kuanzisha msako mkali likishirikiana na kijiji kumsaka mtuhumiwa