Polisi Dodoma kutumia siku 16 kutoa elimu ukatili wa jinsia

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Muktasari:

Jeshi la polisi Dodoma kutumia siku 16 za kupinga ukatili wa jinsia kwa kutoa elimu ya jinsia kwenye vyombo vya usafiri, shule na vijiwe vya mtaani.

Dodoma. Katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limepanga kutoa elimu ya jinsia kwenye vyombo vya usafiri, shuleni na vijiweni.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amesema maeneo hayo ni muhimu kwasababu yapo karibu zaidi na jamii ambazo matukio mengi ya ukatili yamekuwa yakiripotiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari,     Otieno amesema kupitia dawati la jinsia Mkoani hapo askari watawaelimisha watoto kwenye shule zao na vituo vya kulelea watoto yatima kuhusu umuhimu wa kujilinda na kutoa taarifa juu ya viashiria vya ukatili unaowakumba hususan ulawiti na ubakaji.

“Kwa upande wa polisi Mkoa wa Dodoma tunafanya maadhimisho haya kwa kuishirikisha zaidi jamii kwa kufanya mikutano sehemu za jamii kama vile vijiweni, shuleni, nyumba za ibada kupitia madawati yetu ya jinsia,”amesema.

Aidha Kamanda Otieno amesema maadhimisho hayo yatakwenda sambamba na kukutana na wazazi kwaajili ya kutoa elimu ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Pia tutafanya ushirikiano na wenzetu wa Shirikisho la watu wenye ulemavu (Shivyawata) kwaajili ya kuandaa kongamano ambalo litafanyika wilayani Mpwapwa kuhusu masuala ya ukatili,”amesema