Polisi Kiteto wateketeza ekari nne za bangi

Polisi mkoani wilayani kiteto wakikata mmea aina ya bangi katika moja ya shamba lililobainika kufanya shughuli hiyo ambayo ni kinyume na sheria za nchi.

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi wilayani Kiteto, mkoani Manyara, linawashikilia watu kumi akiwemo Tumaini Dornard (25) mkazi wa wilaya ya Kongwa na Rajabu Mta (21) mkazi wa Kijiji cha Matui Kiteto kwa kujihusisha na kilimo cha bangi ekari nne na robo.

Kiteto. Jeshi la Polisi wilayani Kiteto, mkoani Manyara linawashikilia Tumaini Dornard (25) mkazi wa Wilaya ya Kongwa na Rajabu Mta (21) mkazi wa Kijiji cha Matui Kiteto kwa tuhuma kujihusisha na kilimo cha bangi ekari nne na robo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Mei 1, 2023 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi amesema watuhumiwa hao walipanda bangi na mazao mengine katika mashamba hayo ili yasijulikane.

"Ni kweli Jeshi la Polisi Kiteto, tumebaini mashamba mawili ya bangi Aprili 28, 2023 yanayolimwa eneo la Njutaa Kijiji cha Kimana ambayo yanamilikiwa na Tumaini Dornard mkazi wa Kongwa, Mkoa wa Dodoma ambaye anamiliki shamba la ekari nne ambalo alipanda bangi na kuchanganya na mazao mengine yakiwemo mbaazi, alizeti na mahindi,"amesema.

"Pia tulimkamata Rajabu Mta mkazi wa Kijiji cha Matui (21) huyu alikuwa na shamba la robo heka ambalo hakuchanganya na mazao mengine, hivyo bangi hiyo ilikuwa imelimwa yenyewe na ilistawi tayari kwa kuvunwa,"amesema Katabazi

Pia amesema Jeshi la Polisi likishirikiana na wananchi waliteketeza zao hilo akidai taratibu zingine za kisheria zinaendelea kufuatwa

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara tunapambana na dawa za kulevya ikiwemo bangi lakini tumeona sasa twende kwenye vyanzo zaidi huko. Ukamataji kwenye mitaa na vitongozi tu hautoshi tukasema twende zaidi mahali ambako bangi inalimwa tudhibiti huko katika  maeneo hayo,"amesema.

Aidha, Katabazi amesema kwenye misako hiyo wanashirikiana na wananchi ili kuwatambua wahusika wa biashara hizo haramu.