Polisi mkoani Morogoro kutoa elimu kwa madereva

Muktasari:

  • Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Fotunatus Musilimu amewataka madereva wa vyombo vya usafiri kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.

Morogoro. Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Fotunatus Musilimu amewataka madereva wa vyombo vya usafiri kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.

Wito huo ameutoa leo Jumamosi, JUni 12, 2021 mjini Morogoro wakati akizindua kampeni ya safiri salama na kampeni ya safisha wahalifu ambapo amesema ajali nyingi zinazotokea zinasababishwa na madereva kushindwa kufuata sheria za usalama barabarani ikiwemo kuendesha kwa mwendo kasi.

Kamanda Musilimu amesema kupitia kampeni hiyo madereva watapewa elimu inayohusu sheria za usalama barabarani na namna ya kuendesha kwa usalama kwa kuzingatia alama za barabarani.

"Utakuta dereva anaziona alama ya zebra barabarani na kuna watu wanataka kuvuka lakini anashindwa kusimama kuruhusu wapita njia wavuke matokeo yake watembea kwa miguu wanavuka kwa kukimbia jambo ambalo sio sahihi," alisema Musilimu.


Naye mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Morogoro Michael Deleli amesema kuwa ajali nyingi zinazotokea zinasababishwa na mwendokasi wa madereva.

Amewataka abiria hasa wa mabasi kutoa taarifa endepo wataona dereva anaendesha mwendokasi kabla ajali haijatokea ili achukuliwe hatua kali za kisheria.

"Inapotokea ajali ukiwauliza abiria chanzo wengi huwa wanasema ni mwendokasi wa dereva lakini cha kushangaza abiria wanashindwa kutoa taarifa kwa askari wanaokuwa barabarani," alisema kamanda Deleli.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani Joel Kakiziba amesema aliwataka madereva wa bodaboda kuacha kufanya makosa kwa kutegemea kulipa faini ya Sh 10,000 iliyotangazwa na Serikali hivi karibuni na kusema kuwa dereva anaweza kutozwa faini hiyo hata mara tatu kwa siku endapo hatafuata sheria.