Polisi wakamata madumu 1,230 ya mafuta bandari bubu

Muktasari:

Madumu 1,231 ya mafuta ya lita 30 yamekamatwa katika bandari bubu ya Kunduchi jijini Dar es Salaam, kufuatia operesheni ya kikosi cha Polisi Wanamaji.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji kimekamata majahazi matatu yakiwa na shehena ya madumu 1,231 ya lita 20 ya mafuta ya kupikia yakitokea Zanzibar kuelekea bandari bubu Kunduchi.

Madumu hayo yamekamatwa kupitia operesheni zilizokuwa na lengo la kudhibiti uhalifu ukanda wa bahari ya Hindi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la PPolisi iliyotolewa leo Desemba 8, jahazi la kwanza lililotambulika kwa jina SV. Hudallah lililo na namba za za usajili Z. 2523 lilikuwa likiongozwa na nahodha Issa Bakari (26) mkazi wa Bububu Kihinani Zanzibar akiwa na wenzake wanne.

“Jahazi hilo lilikuwa na madumu 500 ya lita 20 aina ya Royal,” imesema taarifa.

Taarifa hiyo pia imetaja jahazi la SV. Wabaya si Wote lenye usajili namba Z.3145 lilikuwa likiongozwa na nahodha Ramadhani Hamisi (42) mkazi wa Uzi Zanzibar akiwa na wenzake 3 huku likiwa na madumu 351 ya lita 20.

"Jahazi la tatu ni SV. Bora Salama lenye usajili namba Z 2946 lilikuwa likiongozwa na Mwalimu Hamisi (40) mkazi wa Uzi Zanzibar akiwa na wenzake wawili, likiwa na madumu 351,"

Wakati operesheni ikiendelea, usiku wakafanikiwa kukamata majahazi mengine mawili, ambayo ni SV Thamarat likiongozwa na Ramadhani Elias (30) mkazi wa Mwanakwerekwe Zanzibar akiwa na wenzake wanne.


"Jahazi hilo lilikuwa limebeba madumu 650 na jahazi lingine SV. Subra ngumu lenye usajili namba Z 3223 likiongozwa na nahodha Juma Shaibu (51) Mkazi wa Mahonda Zanzibar, akiwa na wenzie watatu, likiwa limebeba madumu 500, hivyo kufanya jumla ya madumu ya mafuta yaliyokamatwa kuwa 2381," inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa upelelezi wa awali umeonyesha kuwa mzigo huo ulitakiwa kushuka katika bandari ya Mbweni ambapo taratibu za kulipa ushuru wa forodha zingekamilika na badala yake watuhumiwa hao walielekea katika bandari bubu ya Kunduchi ili kushusha mizigo hiyo.

"Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na Idara nyingine za serikali kuhakiki mzigo huo na baadae taratibu nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Jeshi la Polisi limewapongeza wananchi wanaochukia uhalifu wa aina zote na ambao wanatoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kutokomeza uhalifu.

"Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa wafanyabiashara wasio na uadilifu, kufuata taratibu za mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), la sivyo watakamatwa, na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.”