Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi watumia mabomu kutawanya wamachinga Iringa

Muktasari:

  • Mvutano wa kugawa maeneo ya Machinga katika eneo la Mlandege, Manispaa ya Iringa umeshika kasi baada ya mabomu kutumika kuwatawanya.

Iringa. Jeshi la Polisi Mkoani Iringa leo Machi 14 limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la wamachinga waliohamishiwa eneo jipya la biashara Mlandege, Manispaa ya Iringa.

 Awali Machinga hao walikuwa wakiuza bidhaa zao kati kati ya mji jambo lililoleta mgogoro baina yao na wafanyabiashara wenye maduka.

Hata hivyo kumekuwa na mchakato mrefu katika kugawa maeneo mapya kwa ajili ya wafanyabiashara hao katika eneo la Mlandege ambalo pia lina makaburi ya wazee wa zamani.

Kabla ya mabomu, baadhi ya machinga walirushia mawe gari la polisi lililokuwa limepaki pembezoni mwa barabara, eneo la mzunguko wa barabara za Ipogoro, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Mjini.

Mwananchi ilishuhudia milio ya mabomu kwa lengo la kuwatawanya wafanyabiashara hao walioanzisha vurugu wakati zoezi hilo likiendelea.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi yao walisema baada ya kuhamishwa mjini wanachotaka ni kugawiwa maeneo maalum kwa ajili ya biashara kwani leo ni siku ya nne wamekaa bila kutafuta ridhiki zao.

"Bado hatuelewi tunachotaka kila mtu apewe eneo lakini polisi wanatutishia tunataka kusaidiwa," amesema Amina Nyemba, mmoja wa wafanyabiashara hao.

Pia jopo la Machinga hao wamesema wanaomba viongozi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa awasikilize bila kuwanyima haki zao kama ilivyo sasa.

Kwa upande wa wananchi wamesema suala la Machinga mkoa wa Iringa limekua zito kwa serikali kushindwa kuwaandalia maeneo rasmi ya kufanyia biashara zao na sasa inaleta shida.

"Wangeandaa elimu kwa ajili ya shida hii ila kinachoendelea bila kutatua hakuna tija yoyote" alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wa maeneo karibu na Mlandege wamesema tukio la Machinga limesababisha wao kufunga maduka yao na kushindwa kuendelea na biashara.

Naye Ofisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Janeth Matondo awali alipipigiwa simu aliahidi kumtafuta Meya wa Manispaa hiyo kama yupo ofisini na baadaye hakuweza kupokea simu.

Katibu wa Machinga, Joseph Kilyenyi maarufu kwa jina la Mwanakijiji alisema yupo safari lakini Mwenyekiti hakupokea simu yake.