Polisi yakiri kuua watu watatu Serengeti

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibishiwanu akionyesha bunduki aina ha G3 iliyokamtwa na polisi wakati wa operesheni maalum iliyofanyika wilayani Serengeti na Butiama ambapo watu watatu wamefariki kwa kupigwa risasi na polisi. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limekiri kuwaua raia watatu kwa tuhuma za ujambazi ambao ni wananchi wa Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.

Musoma.  Watu watatu wameuawa kwa kupigwa risasi na askri polisi wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara wakidaiwa kuhusika na vitendo vya ujambazi amabvyo vimekuwa vikitokea katika wilaya za Butiama na Serengeti mkoani humo.

 Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Longinus Tibishiwanu amesema watu hao wamefariki wakiwa njiani kuplekwa hospitalini baada ya kujeruhuwa na risasi walipojaribu kuwatoroka askari polisi.

Tibishiwanu amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Alhamisi Septemba 22, 2022 katika kitongoji cha Gentamome, kijiji cha Majimoto wilayani Serengeti.

Amewataja watu waliofariki ni Mairo Togoro (56), mkazi wa kijiji cha Majimoto, Mwise Simon (54), mkazi wa kijiji Nyamihuru na Mugare Mokiri, mkazi wa kijiji cha Nyamikobiti wote wa wilaya ya Serengeti.

Amesema watu hao pamoja na mwenzao James Mwita (47), walikamatwa Septemba 21, 2022 wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya wizi wa kutumia silaha matukio ambayo yamekuwa yakitokea tangu Juni 2022.

"Matukio kama haya mara ya mwisho yamefanyika kati ya tarehe 4, 10 na 20 mwezi huu na yalifanyika katika vijiji viwili wilayani Serengeti na kimoja wilaya ya Butiama na wakati huo tayari tulikuwa tumeanza kufanya operesheni kwa kushirikiana wenzetu wa Mwanza, Simiyu na Tarime/Rorya," amesema

Amesema katika opresheni hiyo ndipo walipowakamata watu hao wanne ambapo kwa pamoja walikiri kuhusika na vitendo vya ujambazi ambapo waliwataja wenzao watatu wanaoshirikiana nao.

Kamanda huyo amesema, ilipofika usiku askari polisi wakiongozwa na watuhumiwa hao waliondoka kwenda kuwakamata watuhumiwa wengine watatu lakini walipofika katika kitongoji hicho ghafla askari hao walishambuliwa kwa risasi kutoka maporini.

"Askari wakaamua kujibu mashambulizi na wakiwa wanajibizana ndipo hawa watuhumiwa walipojaribu kutoroka lakini askari wetu walifanikiwa kuwapiga risasi watatu kati yao huku mmoja akifanikiwa kutokomea," amesema

Amesema baada ya tukio hilo ndipo watuhumiwa hao walipochukuliwa kwaajili ya kupelekwa hospitalini lakini walifariki wakiwa njiani.

Amesema katika operesheni hiyo askari hao pia walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na bunduki aina ya G3, gobole ambalo limetengenezwa kwa muundo wa pisto pamoja na risasi kadhaa.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamihuru, David Mgendi amesema uisku wa kuamkia Septemba 22, 2022 majira ya saa 9 usiku ilisikika milio ya risasi kwa takriban dakika tano hali iliyosababisha hofu kwa wananchi huku  wakiendelea kukaa ndani kwavile hawakujua kilichokuwa kikiendelea.

"Asubuhi tulienda eneo la tukio karibu na lambo la maji tukakuta damu nyingi sana lakini hadi sasa hatujui kulikuwa na kitu gani na hata ukija sasa hivi utakuta damu zimeganda eneo la tukio," amesema kwa Mgendi alipozungumza kwa simu na Mwananchi Digital

Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), Catherine Ruge amedai miongoni mwa watu waliouawa kwenye tukio hilo ni pamoja na mjomba wake ambaye alikamatwa akiwa nyumabi kwake kijiji cha Majimoto.

Amesema baada ya mjomba wao kukamtwa, leo ndugu zake walikwenda kituo cha polisi Mugumu kilichopo umbali wa zaidi ya kilomita 80 kwaajili ya kumjulia hali pamoja na taratibu zingine lakini mjomba wake huyo hakuwepo kituoni hapo.

"Baada ya kuambiwa hayupo, ndipo ndugu wakaanza kuwasiliana na badaye ikabainika mjomba yupo mochuari na kweli tulipofika hospitalini tulikuta miili ya watu wanne ikiwa imelazwa sakafuni bila nguo na mmoja wapo alikuwa ni mjomba wangu," amesema Ruge kwa njia ya simu.