Polisi yapiga marufuku kununua mifugo kwenye minada ya awali
Muktasari:
- Wanaosafirisha Mifugo nje ya nchi watakiwa kuacha kununua mifugo katika minada ya awali kwa kuwa haitoi vibali na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo, limetoa katazo kwa wafugaji na wafanyabiashara, kuacha tabia ya kununua mifugo kwenye minada ya awali, kisha kuiuza nje ya nchi, likisema kitendo hicho kinaikosesha Serikali mapato.
Badala yake, jeshoi hilo limetaka wanaojishughulisha na biashara hiyo kununua mifugo hiyo katika minada ya upili kwani kwa kufanya hivyo, kunaiwezesha sekta ya mifugo kukua na hivyo kuchangia ukuaji wa pato la taifa.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Oktoba 14, 2023 na Kamanda wa kikosi hicho, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Simon Pasua wakati akizungumza na wafugaji pamoja na wafanyabiashara wa mifugo katika mnada wa Ndala,wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora.
Kamanda Pasua amesema katika minada ya awali havitolewi vibali vya kusafirisha mifugohiyo kwenda nje ya nchi, hivyo waende kwenye minada ya upili ama ya mpakani ambayo ni mikubwa na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo wanapatikana huko kwa ajili ya kutoa vibali.
"Wale wafugaji na wafanyabiashara wenye utamaduni wa kutegemea minada ya awali kununua mifugo na kusafirisha kwenda nje ya nchi kuuza, wanapaswa kuacha na badala yake wakanunue kwenye minada ya upili inayotoa vibali vya kusafirisha mifugo kwenda nje ya nchi," amesema.
ACP Pasua amebainisha kuwa kwa wale watabainika kusafirisha mifugo hiyo bila kufuata utaratibu kwa kukwepa kulipa ushuru ama kutokuwa na vibali, hatua za kisheria dhidi yao zitachuliwa na jeshi hilo, ikiwa ni pamoja na kukamata mifugo hiyo na kuwafikisha Mahakamani.
"Jeshi linaendelea kutoa elimu katika minada yote nchini pamoja na mambo mengine wafugaji mnaelimishwa namna bora ya kufanya biashara bila kununua mifugo ya wizi ama ile yenye migogoro," amesema
Kwa upande wake Methew Kabundala kwa niaba ya wafugaji amesema kuwa tatizo linalowakabili katika mnada hiyo ni mifugo kuwa mingi zaidi ya miundombinu ya mazizi hali inayosababisha biashara kufanyika nje.
"Tunaomba Serikali kuboresha mazingira ya mnada ili uweze kukidhi mahitaji, na kuvutia watu wengi kujitokeza kununua na Serikali kupata mapato," amesema.